31 May 2011

Tuishi Kiislam

Tofauti yetu na wasio kuwa Waislam si chengine kipya ila ni tabia. Uzuri wa mwenendo wa maisha yetu ndio utakaotupatia sifa mbele ya jamii isiyokuwa ya Waislam. Hima yetu ya kutosema uongo na kufuata maadili ya ajabu ndio utakuwa msingi imara wa imani yetu. Haya yote yameelezwa na Habiybul Mustwafaa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa hakuletwa yeye isipokuwa kurekebisha jamii kuwa na tabia njema.

Hakika Uislamu wetu umekamilika kwa kuwa na tabia bora za kuigwa na Waislam wenyewe kwa ushahidi wa Qur-aan na Sunnah.

Kama kweli sisi ni Waislam tunaoipenda diyn yetu ni lazima tuwe tayari kuanza kubadilika kila hatua ya maisha yetu kwa kuishi Kiislam. Zingatio letu litatupeleka hatua baada ya hatua ili kurekebisha nyumba iliyojikita kwenye masuala yasioendana kabisa na mila zetu sisi Waislam.


1. TUZUNGUMZE KIISLAM

Muislam wa kweli ni lazima awe ni mkweli, hatakiwi kuzua uongo, kufitinisha, kusengenya wala kuzungumza kwa sauti ya juu. Haya tunayapata ndani ya Qur-aan:

{{Na uteremshe sauti yako; bila shaka sauti ya punda ni mbaya kuliko sauti zote (kwa makelele yake ya bure).}} [Surat Luqmaan: 19]

Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana kushikamana katika kusema ukweli:

“Shikamaneni na ukweli, kwani ukweli unapeleka katika wema, na wema unapeleka Peponi.” [Muslim]


2. TULE KIISLAM

Muislam anatakiwa ale kilicho mbele yake kwa kutumia mkono wa kulia na asiwe na papara ya kusukuma tonge namna ya kima anavyokula. Aanze kula kwa kusema “BismiLlaah” na amalize kwa kusema “AlhamduliLlaah”. Chakula cha Muislam ni lazima kiwe ni cha halali, hatakiwi kula ovyo ovyo kama wanavyofanya wasiokuwa Waislam. Anapokula aligawe tumbo lake kwenye thuluthi tatu. Thuluthi moja ni ya chakula, nyengine ni ya maji na mwisho ni hewa. Hii ni kwa mujibu wa dalili ya Hadityh:

"Kama ukilazimika kula hakikisha theluthi moja ya tumbo lako unaijaza chakula, theluthi moja maji na acha theluthi moja kwa ajili ya hewa (yaani iache tupu)” (At-Tirmidhiy).


3. TUSIKILIZE KIISLAM

Muziki ni haramu na haifai kwa Muislam kuutengeneza, kutengenezewa, kuimba, kuimbiwa, kuutangaza, kuupeleka muziki, kuuza, kula thamani yake, kununua na kuuza. Muziki umekuwa ni tatizo kubwa kwa Waislam kwani wengine hata usingizi hawapati bila ya kusikiliza muziki. Nyumba za Kiislam sasa zimekuwa sawa na magofu kwa kutopatikana maadili ya Kiislam. Kwani wengi wanaishi tofauti na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni muhimu kwa Waislam wakawa wanasoma Qur-aan kila siku kwa sauti na kwa kusikilizana kwa mtindo wa dawaar (mmoja baada ya mwengine). Tuzibadilishe nyumba zetu kwa kusikiliza idhaa za Kiislam zisizokuwa na mambo ya uchafu na uzushi.

((Na soma Qur-aan kwa utaratibu na utungo))  [Al-Muzammil 73: 4]

Muislam anayesoma Qur-aan atakuwa pamoja na Malaika na Mitume (‘Alayhi swalaatu was-salaam). Hata yule asiyejua kusoma Qur-aan ni vyema akawa na jitihada ya kujifundisha ilhali anakosea au hata kuchekwa. Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Yule ambaye kwamba anasoma Qur-aan naye ni mjuzi (hana shida aina yoyote) atakuwa pamoja na Malaika na Mitume (‘Alayhi swalaatu was-salaam) na watiifu. Na yule ambaye kwamba anarudia pamoja na kuwa na shida katika kusoma basi atakuwa na ujira mara mbili(( [al-Bukhaariy, Muslim, Tirmidhy na Ibn Maajah kutoka kwa ‘Aishah (Radhiya Allaahu 'anha)]


4. TUVAE NA TUTEMBEE KIISLAM

Maringo ya kutembea bila ya shaka yanatokana na mtu kuvaa nguo za kifakhari ambazo hazitakiwi kuvaliwa kwa Muislam. Muislam wa kiume anatakiwa avae nguo zisizoburura. Mwanamke hatakiwi kuonekana zaidi ya viganja vya mikono na kipaji cha sura yake. Mapambo yote ni halali kwa mumewe na walio Maharimu wake. Haitakikani Muislam kutembea kwa kujivuna, kujifakharisha na maringo. Hivi sivyo Uislam unavyotufundisha kuishi. Qur-aan inasema:

{{Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala huwezi kufikia urefu wa milima}} [Surat Israa: 37]

Usiwaangalie watu kwa jeuri au kwa upande mmoja wa uso. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

{{Wala usiwatazame (usiwafanyie watu jeuri), kwa upande mmoja wa uso, wala usende katika ardhi kwa maringo, hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila ajivunaye, ajifaharishaye.}} [Surat Luqmaan:18]
                                      

5. TUJENGE URAFIKI WA KIISLAM

Miongoni mwa matatizo makubwa ya vijana wetu pamoja na Waislam kukosa maadili ya Kiislam ni kuwa na marafiki wasiokuwa na maadili mema. Ni vyema Muislam akawa hana rafiki hata mmoja kuliko kuwa na marafiki kumi wasioishi Kiislam. Kuishi Kiislam yatakikana juhudi na inaanza kwa kuwa na rafiki mwema atakayekukemea unapofanya kosa na kukupa maneno ya subra wakati wa huzuni.

Lazima tuchague marafiki ambao wako radhi na dini yetu na tuepukane na wale ambao hawako radhi na dini yetu. Na tukiona marafiki zetu matendo yao sio mazuri, ni lazima tuepukane nao kwa sababu tunaweza tukaiga tabia zao ambazo zinakwenda kinyume na dini yetu.
Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mtu yamkini kufuata dini ya rafiki yake, kwa hivyo muangalie unayemfanya rafiki.”  (Abuu Daawuud na Tirmidhiy)

6. TULALE KIISLAM

Tumalizie kwa kuona namna anavyotakiwa Muislam kuimaliza siku yake kwa kujipumzisha Kiislam. Muislam anatakiwa atie wudhuu kabla ya kulala, wudhuu unaendana na Sunnah ya kupiga mswaki. Ni vizuri ukaswali rakaa tatu za witri (kwa wasioamka usiku).

Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akienda kulala usiku anakusanya viganja vyake kisha akivipuliza na akivisomea Suratul-Ikhlaas, na Suratul-Falaq, na Suratu-Nnaas, kisha akipangusa kwa hivyo viganja vyake kiasi anachoweza katika mwili wake, akianza kichwani na usoni na mbele (akifanya hivyo mara tatu).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ukienda kulala soma Ayatul-Kursiy mpaka uimalize kwani Mwenyezi Mungu Ataendelea kukuhifadhi wala hakukaribii shetani mpaka asubuhi”
Unapolala ulaze ubavu kwa upande wa kulia na usome du’aa ifuatayo:

اللّهُـمَّ أَسْـلَمْتُ نَفْـسي إِلَـيْكَ، وَفَوَّضْـتُ أَمْـري إِلَـيْكَ، وَوَجَّـهْتُ وا جْـهي إِلَـيْكَ، وَأَلْـجَـاْتُ ظَهـري إِلَـيْكَ، رَغْبَـةً وَرَهْـبَةً إِلَـيْكَ، لا مَلْجَـأَ وَلا مَنْـجـا مِنْـكَ إِلاّ إِلَـيْكَ، آمَنْـتُ بِكِتـابِكَ الّـذي أَنْزَلْـتَ وَبِنَبِـيِّـكَ الّـذي أَرْسَلْـت
“Ewe Mwenyezi Mungu  nimeisalimisha nafsi yangu kwako, na nimekuachia mambo yangu Wewe na nimeuelekeza uso wangu kwako na nimeutegemeza mgongo wangu kwako, kwa matarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila kwako, nimekiamini kitabu chako ulichokiteremsha na Mtume wako uliyemtuma”.
Bila ya shaka tutakapoishi Kiislam tutakuwa mbali na wasiokuwa Waislam. Hivyo maisha yetu yatakuwa hakika ni ya Kiislam. Kila kitu yatakikana juhudi na inaanza kwa nafsi kujifunga kukubali mafundisho ya Kiislam. Inawezekana kubadilika kwa kuishi Kiislam. Anza sasa, katu usichelewe kuishi Kiislam.

 Nyiradi za kulala
(99)
Alikuwa Mtume صلى الله عليه وسلم akienda kulala usiku anakusanya viganja vyake kisha akivipuliza na akivisomea Suratul-Ikhlaas, na Suratul-Falaq, na Suratu-Nnas, kisha akipangusa kwa hivyo viganja vyake kiasi anachoweza katika mwili wake, akianza kichwani na usoni na mbele .
(akifanya hivyo mara tatu)

(100)
Mtume صلى الله عليه وسلم amesema : “Ukienda kulala soma Ayatul-Kursiy mpaka uimalize kwani  Mwenyezi Mungu  ataendelea kukuhifadhi wala hakukaribii shetani mpaka asubuhi”
)اللّهُ لا إلهَ إلاّ هُـوَ الـحَيُّ القَيّـومُ لا تَأْخُـذُهُ سِنَـةٌ وَلا نَـوْمٌ …..(
(Suratul Baqara -255)

(101)
Amesema Mtume صلى  الله عليه وسلم“Anaesoma aya mbili za mwisho wa Suratul-Baqarah usiku zinamtosheleza"
(آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ كُلٌّ آمَنَ بِاللّهِ وَمَلآئِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لاَ نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ وَقَالُواْ سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ ) ( لاَ يُكَلِّفُ اللّهُ نَفْسًا إِلاَّ وُسْعَهَا لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ رَبَّنَا لاَ تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا رَبَّنَا وَلاَ تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا رَبَّنَا وَلاَ تُحَمِّلْنَا مَا لاَ طَاقَةَ لَنَا بِهِ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَآ أَنتَ مَوْلاَنَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِين)
(Suratul Baqarah 285-286)

(102)
Mtume صلى الله عليه وسلم pia amesema : “Akiamka mmoja wenu kutoka usingizini kisha akarudi basi akikukute kitanda kwa shuka yake mara tatu na amtaje Mwenyezi Mungu  kwani hajui kilicho kuja baada yake.  Na Akilala aseme:
بِاسْمِكَ رَبِّـي وَضَعْـتُ جَنْـبي ، وَبِكَ أَرْفَعُـه، فَإِن أَمْسَـكْتَ نَفْسـي فارْحَـمْها ، وَإِنْ أَرْسَلْتَـها فاحْفَظْـها بِمـا تَحْفَـظُ بِه عِبـادَكَ الصّـالِحـين
“Kwa jina lako Mola wangu, nimeweka ubavu wangu na kwa ajili yako nitaunyanyua, na ukiizuia (ukiichukuwa) roho yangu basi  irehemu na ukiirudisha basi ihifadhi kwa kile unacho wahifadhi nacho waja wako wema”
(103)
اللّهُـمَّ  إِنَّـكَ خَلَـقْتَ نَفْسـي  وَأَنْـتَ تَوَفّـاهـا لَكَ ممَـاتـها وَمَحْـياها ، إِنْ أَحْيَيْـتَها فاحْفَظْـها ، وَإِنْ أَمَتَّـها فَاغْفِـرْ لَـها . اللّهُـمَّ  إِنَّـي أَسْـأَلُـكَ العـافِـيَة
“Ewe Mwenyezi Mungu  hakika Wewe umeiumba nafsi yangu nawe utaiua, ni kwako uhai wa nafsi yangu na ufaji wake, ukiipa uhai basi ihifadhi, na ukiifisha (ukiiua) basi isamehe.  Ewe Mwenyezi Mungu  hakika mimi nakuomba afya njema”

(104)
Alikuwa Mtume صلى الله عليه وسلم akitaka kulala anaweka mkono wake wa kulia chini ya shavu lake  kisha anasema:
اللّهُـمَّ قِنـي عَذابَـكَ يَـوْمَ تَبْـعَثُ عِبـادَك
“Ewe Mwenyezi Mungu  nikinge mimi kwa adhabu yako siku utakayo wafufua waja wako”
(mara tatu)

(105)
بِاسْـمِكَ اللّهُـمَّ أَمـوتُ وَأَحْـيا
“Kwa jina lako Ewe Mwenyezi Mungu  ninakufa na ninakuwa hai”
(106)
Mtume صلى الله عليه وسلم amesema : “Hivi  niwafahamishe juu ya kitu ambacho ni bora zaidi kuliko mtumishi wakati munapolala;  Msabihini Mwenyezi Mungu   mara thelathini na tatu, kisha msifuni Mwenyezi Mungu  mara thelathini na tatu, na kisha mtukuzeni mara thelathini na tatu kwani kufanya hivi ni bora kwenu kuliko mtumishi”
سُبْـحانَ الله
“Ametakasika Mwenyezi Mungu"
(Mara thelathini na tatu )
 أَلْحَمْدُ لِلَّه
“Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu"
(Mara thelathini na tatu )
اللَّه أكْبَرُ
“Mwenyezi Mungu  Mkubwa”
(Mara thelathini na tatu )

(107)
اللّهُـمَّ رَبَّ السّمـواتِ السَّبْـعِ وَرَبَّ العَـرْشِ العَظـيم ، رَبَّنـا وَرَبَّ كُـلِّ شَـيء ، فالِـقَ الحَـبِّ وَالنَّـوى ، وَمُـنَزِّلَ التَّـوْراةِ وَالإنْجـيل ، والفُـرْقان ، أَعـوذُ بِـكَ مِن شَـرِّ كُـلِّ شَـيءٍ أَنْـتَ آخِـذٌ بِنـاصِـيَتِه . اللّهُـمَّ أَنْـتَ الأوَّلُ فَلَـيسَ قَبْـلَكَ شَيء ، وَأَنْـتَ الآخِـرُفَلَـيسَ بَعْـدَكَ شَيء ، وَأَنْـتَ الظّـاهِـرُفَلَـيْسَ فَـوْقَـكَ شَيء ، وَأَنْـتَ الْبـاطِـنُ فَلَـيْسَ دونَـكَ شَيء ، اقـْضِ عَنّـا الـدَّيْـنَ وَأَغْـنِنـا مِنَ الفَـقْر
“Ewe Mwenyezi Mungu  Mola wa mbingu saba na Mola wa arshi tukufu, Mola wetu na Mola wa kila kitu Mwenye kuichanua tembe ya mbegu na kokwa na alieteremsha Taurat na Ijiil na Qur’ani, najikinga kwako kutokana na shari ya kila kitu.   Wewe  ndie mwenye kukamata utosi wake. Ewe Mwenyezi Mungu  Wewe ndie wa Mwanzo hakuna kabla yako kitu, nawe ndie wa Mwisho,hakuna baada yako kitu, nawewe ndie uliewazi, hakuna juu yako kitu chochote na Wewe ndie uliefichika hakuna kilichojificha chini yako. Tulipie madeni yetu na utuepushe na ufakiri”

(108)
الـحَمْدُ للهِ الَّذي أَطْـعَمَنا وَسَقـانا، وَكَفـانا، وَآوانا، فَكَـمْ مِمَّـنْ لا كـافِيَ لَـهُ وَلا مُـؤْوي
“Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu  ambae ametulisha na ametunywesha na akatutosheleza na akatuhifadhi, ni wangapi ambao hawana wa kuwatosheleza wala wa kuwahifadhi”

(109)
اللّهُـمَّ عالِـمَ الغَـيبِ وَالشّـهادةِ فاطِـرَ السّماواتِ وَالأرْضِ رَبَّ كُـلِّ شَـيءٍ وَمَليـكَه، أَشْهـدُ أَنْ لا إِلـهَ إِلاّ أَنْت، أَعـوذُ بِكَ مِن شَـرِّ   نَفْسـي، وَمِن شَـرِّ الشَّيْـطانِ وَشِـرْكِه، وَأَنْ أَقْتَـرِفَ عَلـى  نَفْسـي  سوءاً أَوْ أَجُـرَّهُ إِلـى مُسْـلِم .
“Ewe Mwenyezi Mungu mjuzi wa yaliyojificha na yaliyowazi, Muumba wa mbingu na ardhi, mola wa kila kitu na Mfalme wake, nakiri kwamba hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe, najilinda kwako na shari ya nafsi yangu na shari ya shetani na shirki yake na kujichumia uovu kwa nafsi yangu au kumletea Muislamu.

(110)
Mtume صلى الله عليه وسلم alikuwa halali mpaka asome Suratu-Sajda na Suratul-Mulk .

 Ukitaka kulala tawadha udhu kama wa swala kisha lalia ubavu wako wa kulia kisha sema :
اللّهُـمَّ أَسْـلَمْتُ نَفْـسي إِلَـيْكَ، وَفَوَّضْـتُ أَمْـري إِلَـيْكَ، وَوَجَّـهْتُ وَجْـهي إِلَـيْكَ، وَأَلْـجَـاْتُ ظَهـري إِلَـيْكَ، رَغْبَـةً وَرَهْـبَةً إِلَـيْكَ، لا مَلْجَـأَ وَلا مَنْـجـا مِنْـكَ إِلاّ إِلَـيْكَ، آمَنْـتُ بِكِتـابِكَ الّـذي أَنْزَلْـتَ وَبِنَبِـيِّـكَ الّـذي أَرْسَلْـت
“Ewe Mwenyezi Mungu  nimeisalimisha nafsi yangu kwako, na nimekuachia mambo yangu Wewe na nime uelekeza uso wangu kwako na nimeutegemeza mgongo wangu kwako, kwa matajarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila kwako, nimekiamini kitabu chako ulicho kiteremsha na Mtume wako uliyemtuma”

Ameseme Mtume صلى الله عليه وسلم ‘kwa mwenye kusema haya kisha ukifa utakuwa umekufa katika Uislamu’

Aina Za Ndoa Na Hukumu Zake

Abu ‘Ammaar
Katika makala hii fupi inshaAllaah tutajaribu kuzitambulisha aina za ndoa na kuweza kuzijua hukumu zake kisheria pamoja na maelezo kwa ufupi.

Ndoa ni mkataba unaofungwa na wanandoa kuhalalisha kila mmoja wao kuweza kustarehe na mwengine kwa mujibu wa sheria.

Ndoa ni miongoni mwa alama na miujiza yake Allaah (Subhaanahu Wata’ala) na ina dalili ya kuthibitika kwake katika Qur’aan na katika Sunnah.

Katika Qur’aan
Suuratu Nnisaa/3
 وَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تُقْسِطُواْ فِي الْيَتَامَى فَانكِحُواْ مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَى وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُم
“Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne. Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki.”

Suuratu Nnuur/32
وَأَنكِحُوا الْأَيَامَى مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُم
“Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu.”


Katika Sunnah
يامعشر الشباب ، من استطاع منكم الباءة فليتزوج فإنه أغض للبصر  وأحصن للفرج ، ومن لم يستطع فعليه  بالصوم فإنه له وجاء
 أخرجه البخاري
“Enyi vijana! Mwenye uwezo wa kuisimamia ndoa na aoe kwani huko ni kuweza kuinamisha macho na kuweza kuzikinga tupu na kama hamna uwezo basi ni juu yenu kufunga kwani huko ndiko kwenye kinga.” Al-Bukhaariy
Na pia:
النكاح من سنتي ، فمن لم يعمل بسنتي فليس مني
Ndoa ni miongoni mwa Sunnah zangu na mwenye kutenda kinyume na Sunnah zangu hatokuwa pamoja na mimi. Ibn Maajah

Ili ndoa ikamilike hupaswa kutimiza nguzo, masharti pamoja na adabu zake vinginevyo inaweza kuwa miongoni mwa ndoa zenye utata katika uhalali wake.

Ndoa, kwa mujibu wa Rai za Jamhuur Ulamaa (isipokuwa Abu Haniyfah), zimegawika kwenye sehemu kuu tatu zifuatazo:

1       Ndoa sahihi iliyokamilika
Iliyotimiza nguzo na masharti ya kusihi kwake na kuweza kutekelezwa.

2       Ndoa Sahihi isiyokamilika
Iliyotimiza nguzo na masharti ya kusihi kwake lakini imeshindwa kutekelezwa.

3       Ndoa batili au fasidi
Iliyokosekana moja ya nguzo au masharti ya kusihi kwake.


Yanayopaswa kuwepo wakati wa kufungwa ndoa (Aqdi)
Ni yafuatayo:

1       Kuwepo mke na mume (ambao wataweza kuisimamia ndoa na kutokuwepo vizuizi vya kuwazuia kuoana)-miongoni mwa masharti ya ndoa.

2       Ijaabu (tamko la kuoa au kuozesha) na Qabuul (tamko la kukubali) - miongoni mwa nguzo za ndoa

3       Awepo walii -miongoni mwa masharti ya ndoa

4       Wawepo Mashahidi - miongoni mwa masharti ya ndoa

Yanayopaswa kuzingatiwa
Ni yafuatayo:

·         Asiwe mmoja wa wanandoa ana vizuizi vya kuwafanya wasioane ikiwa ni vya muda au vya kudumu.

·         Mkataba wa ndoa uwe wa kudumu usiwekewe muda maalum.

·         Ridhaa, chaguo na uamuzi uwe ni wa wanandoa kusiwepo kulazimishana.

·         Wasiwe wanandoa katika hali ya kuhirimia kwa ajili ya Hajj au ’Umrah.

·         Yawepo mahari.

·         Wajulikane wanaooa au kuolewa.

·         Kusiwepo mbinu za kutoitangaza ndoa na kuificha.

Ndoa batili au fasidi


1
NDOA FASIDI/ BATILI
Iliyofisidika kwa kukosekana moja katika nguzo, masharti ya msingi ya kufungika ndoa.
Ndoa hutakiwa ikamilike mambo yake yote zikiwemo nguzo masharti ya kusihi kwake ili iweze kuwa na uhalali kisheria.
Haijuzu
2
NDOA WAKATI WA IHRAAMU
Kuoa/kuolewa wakati mmeshahirimia ima kwa ibadah ya Hajj au ‘Umrah.
Kuwepo katika hali ya Ihraamu ni moja katika mambo yanayomzuia mke/mume kufanya tendo la ndoa na kuoa au kuwakilishwa ndoa pia ni mambo yasiyofanywa kwa aliye kwenye Ihraamu.
Haijuzu
3
NDOA BILA YA WALII
Kufungwa ndoa kwa kuwepo mke na mume pamoja na mashahidi lakini Walii amekosekana.
Ndoa haikamiliki bila ya kuwepo kwa Walii na ni mojawapo ya nguzo za ndoa. Walii ni mwenye haki ya kumuozesha na kusimamia ndoa kwa niaba ya binti.
Haijuzu kwa mujibu wa Jamhuur Ulamaa na inajuzu kwa mwanamke aliye baleghe kujiozesha kwa mujibu wa rai ya Abu Haniyfah.
4
NDOA YA “WALII” ASIYEKUWA NA SIFA
Kufungwa ndoa kwa kutimizwa masharti yote isipokuwa walii ni mama wa binti kwa kukosekana baba na mfano wake.
Moja katika masharti ya kusihi ndoa ni kuwepo walii mwanamme. Kisheria walii ni mwanamme na mwanamke si miongoni mwa walii wa binti.
Haijuzu
5
NDOA BILA YA KUWEPO MASHAHIDI
Kufungwa ndoa wakiwepo mke na mume na walii bila ya kuwepo shahidi kama ilivyo ndoa ya Mut’ah au ndoa ya siri
Ni moja katika masharti ya kusihi ndoa kwamba lazima ishuhudishwe na mashahidi ili kuondosha dhana ya kuwepo ndoa za siri na kuondosha tuhuma na dhana.
Haijuzu




Ndoa zenye utata katika kujuzu kwake



NDOA
MAELEZO
SABABU
HUKUMU
1
NDOA YA MUT’AH (MUDA MAALUM)
Hufungwa kwa muda maalum japo masaa mawili, bila mashahidi wala walii, ambapo wanandoa kuwa na haki kama wameoana.
Imewekewa muda maalum na hakuna kurithiana wala kutalikiana.
Haijuzu
2
NDOA YA MHALILI (ALIYEACHIKA TALAKA TATU)
Kuolewa mke aliyeachika talaka tatu si kwa lengo la ndoa bali kwa lengo la kuipinda sheria ili ahalalishiwe mume wa mwanzo.
Mume anataka kurudiana na mkewe ambaye kamuacha talaka tatu na hivyo kumtafuta mume mwengine amuoe mkewe kwa makubaliano lakini pasipatikane tendo la ndoa kisha amuache.
Kisheria atatakiwa aolewe na mume mwengine ndoa halisi na papatikane tendo la ndoa.
Haijuzu
3
NDOA ZAIDI YA WAKE WANE
Mume kuoa wake zaidi ya wane kwa wakati mmoja waliokubalika kisheria.
Ruhusa na mipaka tuliyowekewa na sheria ni kuwa na wake wane tu kwa wakati mmoja. (Na hata kama mke  ameachika talaka rejea  na yupo katika eda basi uharamu upo pale pale).
Haijuzu
4
KUOLEWA NA MUME ZAIDI YA MMOJA  WAKATI MMOJA
Mke kuolewa na mume zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja yaani kuwa na waume wawili na kuendelea.
Sheria inakataza mke kuolewa na waume wengi kwa wakati mmoja kwani ni kinyume na fitrah- maumbile ya asli (Uislamu).
Haijuzu
5
NDOA KWENYE EDA
Kumuoa au hata kumposa mke aliyeachika na bado yupo katika eda na hakuwa mke wake kabla.
Kuwepo kwenye eda ya aina yoyote kwa mke ni kizuizi kinachomfunga kutoweza kuolewa mpaka imalizike isipokuwa kwa mtalaka wake tu kama mke aliyeachika talaka rejea.
Haijuzu
6
NDOA KWENYE UJA UZITO KWA MWANAMKE AMBAYE HAJAPATA KUOLEWA KABLA
Kwa mwanamke ambaye hajaolewa akazini na kupatikana ujauzito na kutaka kuolewa katika hali hii. Ndoa hizi hufanyika pale mambo yameshaharibika na kutaka kusitiriana
Ujauzito utakuwa na hukumu sawa kama mwanamke aliye katika eda (Ahmad na Abu Haniyfah). Uja uzito hautokuwa na hukumu sawa kama mwanamke aliye katika eda (Maalik na ash-Shafi’iy).
Haijuzu kwa rai ya Ahmad na Abu Haniyfah
Inajuzu kwa rai ya Maalik na ash-Shafi’iy ila tu hatopaswa kustarehe naye mpaka ajifungue.
7
NDOA KWENYE UJA UZITO KWA ALIYEACHIKA
Mke aliyeachika na ni mja mzito na kutaka kuolewa na mume mwengine asiyekuwa mtaliki wake.
Mke aliyeachika katika uja uzito yupo katika Eda na humalizika atakapojifungua na kumaliza muda wake wa Nifasi. Kisheria Eda  inamfunga mke  kuolewa mpaka imalizike.
Haijuzu
8
NDOA KWA ASIYEKUWA MUISLAMU WALA HAKUTEREMSHIWA KITABU

Kuoa washirikina  na makafiri ambao si miongoni mwa walioteremshiwa vitabu kama mayahudi na manasara.
Moja katika masharti ya kusihi ndoa ni Uislamu. Hivyo kuoa asiyekuwa Muislamu huifanya ndoa kuwa fasidi.
Haijuzu
9
NDOA KWA ASIYE MUISLAMU LAKINI NI MIONGONI MWA WALIOTEREMSHIWA KITABU
Walioteremshiwa vitabu miongoni mwa mayahudi na manasara na wanaowafuata katika mila zao.
Uislamu ni moja ya masharti ya kusihi ndoa ila kwa mujibu wa aya za Qur’aan wameruhusika kuolewa.
Inajuzu ingawa ni Makruuh - haipendezi
10
KUOLEWA MUISLAMU NA ASIYEKUWA MUISLAMU
Mwanamke wa Kiislamu kuolewa na kafiri, mwenye kumshirikisha Allaah pamoja na mayahudi na manasara.
Ndoa hulazimisha utiifu wa mke kwa  mumewe na hivyo kuwepo khofu ya kuweza kuathirika na kubadilisha dini na watoto kufuata dini ya baba.

Haijuzu
11
KUOA/KUOLEWA NA ALIYERTADI
Mwanamme au mwanamke aliyekuwa Muislamu kisha akaamua kurtadi – kutoka katika dini.
Kwa kukosekana sharti la msingi la Uislamu na hata kama atakuwa amekwenda katika dini ya walioteremshiwa vitabu.
Haijuzu
12
KUMUOA BINTI ULIYEZAA NJE YA NDOA
Mwanamme kuoa binti aliyezaa baada kutembea (kuzini) na mama yake nje ya ndoa.
Huyu ni mtoto wake kwani ni mbegu zake ila tu atakosa baadhi ya haki za kimsingi kwa kuzaliwa nje ya ndoa.
Haijuzu
13
KUOA BINTI WA KAMBO AMBAYE MLIWAHI KUWA NA MAHUSIANO HARAMU NA MAMA YAKE
Kuoa binti wa kambo ambaye mliwahi kuwa na uhusiano haramu (zinaa) na mama yake kabla. Si binti aliyezaa nje ya ndoa bali ni binti wa mama.
Kutokana na kupatikana tendo la haramu la zinaa Maulamaa wametofautiana katika tendo hili (zinaa) je llitaweza kuharamisha halali (ndoa)? Na kuna Qaaidah-“Haramu haiwezi kuifanya halali nyengine kuwa haramu”. Kuna Qaaidah nyengine “tendo la haramu huharamisha halali”.

Inajuzu kwa rai ya ash-Shaafi’iy na Maalik kwa sababu ya kutokuwepo dalili bayana kuharamisha. Haijuzu kwa rai ya Abu Haniyfah na Ahmad bin Hanbal kwa sababu ya kuwepo tendo la haramu zinaa. 
14
KUOA BINTI WA KAMBO AMBAYE MLIWAHI KUWA NA MAHUSIANO HALALI NA MAMA YAKE
Kuoa binti wa kambo ambaye kuliwahi kuwepo mahusiano ya halali (ndoa) na mama yake mzazi na binti huyu si miongoni mwa watoto wa mume.

Haijuzu

15
KUOA MAMA AMBAYE ULIWAHI KUOA BINTI YAKE
Kumuoa mama ambaye kabla mliwahi kuwa na uhusiano wa ndoa na binti yake.
Haijuzu
16
NDOA KWA WALIONYONYA ZIWA MOJA
Ikiwa watoto wa kike na wa kiume wametokezea kunyonya ziwa moja kwa mama mmoja na wakataka kuoana.
Moja katika mambo yanayoharamisha ndoa ni kuoa /kuolewa na mliyenyonya ziwa moja kwani kitendo hiki tayari kisheria kimeshaunda udugu baina yao.
Haijuzu
17
NDOA YA KUBADILISHANA (SHIGHAAR)
Mwanamme kumuozesha binti/dada yake kwa mwanamme mwengine ambaye naye atamuozesha binti/dada yake kwa mwanamme wa mwanzo kwa mabadilishano.
Ndoa hizi hufanyika pasi na kutajwa mahari kwani mahari ya kila mmoja ni kumkubalia mwengine kuoa kwake “nipe nikupe” na pasi na kupatikana ridhaa ya upande mwengine.
Rai yenye nguvu haijuzu kwa kufanyika kinyume na misingi ya ndoa ya Kiislamu.
18
NDOA YA BOMANI
Ndoa zinazofungishwa na wakuu wa wilaya au kwenye ofisi za wasajili wa ndoa serikalini.
Hufanyika bila ya kutekelezwa masharti ya kimsingi katika sheria za ndoa za Kiislamu kwani si lazima kuwepo mashahidi au kuwa wanandoa ni wa dini moja.
Haijuzu.

Ikiwa taratibu za nchi zinahitaji kufungwa ndoa hii itawajibika kwanza kufungwa ndoa ya Kiislamu.
19
NDOA YA MISYAAR
Mwanamke hukubali kuolewa huku akisamehe baadhi ya haki zake za kimsingi katika ndoa kama mahari, huduma na makaazi au hata katika kugawana siku (kwa wake wenza).
Ndoa hizi hufanyika sana katika Bara Arabu hasa kutokana na ughali wa mahari na hivyo mke katika kutafuta stara huzisamehe baadhi ya haki zake.
Na pia kama wenye kuoa Afrika huku wakiwa na mke mwengine na hivyo mke wa Afrika kusamehe baadhi ya haki zake kama za kugawana siku na nyenginezo kwa kuwa anapata huduma nyengine kama pesa na kadhalika.
Itajuzu ikiwa  imetimiza masharti ya kimsingi – Haitojuzu ikiwa haitotimiza masharti ya kimsingi kama kufanyika ndoa ya Misyaar bila ya Walii.
20
NDOA YA MISFAAR
Hufungwa kwa muda maalum kama wakati wa mapumziko au kwa wafanyakazi, wanafunzi ambao wako mbali na miji au nchi zao humalizika baada ya kurudi sehemu zao walikotoka
Kimsingi ndoa yoyote itakayowekewa mkataba/muda maalum kumalizika kwake haikubaliki kisheria kama ilivyo Mut’ah. Mfano wanandoa wamekubaliana kuoana wakiwa Uingereza tu lakini wakirudi walipotoka ndoa imemalizika hata bila ya talaka.
Haijuzu kwa rai ya Jamhuur
Licha ya kutimiza masharti yote ya kimsingi ila kwa kuwepo muwafaka wa kumalizika kwake ambao ni kinyume na taratibu za ndoa ya Kiislamu.
Itajuzu kwa rai ya Abu Haniyfah ikiwa sharti la kumalizika halitozingatiwa kwani ni sharti batili.

21
KUOA MWANAMKE ALIYEPOSWA KABLA
Kuvunja uchumba uliopo na kuposa kisha kumuoa binti ambaye tayari ameshachumbiwa.
Kwenda kuposa mwanamke aliyeposwa ni haramu kisheria. Kwa mujibu wa Hadithi za Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Ikiwa atakayeposa anajua taarifa za kuposwa kwa binti kabla basi
mtendaji ni mwenye madhambi na dhimma kwa kukiuka makatazo.
Kama hakujua na kufahamu baadae basi uharamu upo pale pale
Ndoa itajuzu kwa mujibu wa rai ya Jamhuur Ulamaa kwa sababu kilicho haramu kilitokea kabla ya kufungwa na si katika ndoa kwani khutba si miongoni mwa mwa masharti ya kusihi ndoa.

Haijuzu kwa mujibu wa Maalik na kama ndoa itafanyika itabidi ibatilishwe

22
NDOA YA KUJIFICHA  “SIRI”
Kuoana kwa kukamilisha nguzo na masharti yote ya ndoa ila tu wanandoa na mashahidi kutakiwa kutoitangaza na kuidhihirsha.
Ikiwa ndoa hii itakamilika katika idara zote ila kilichokosekana ni mashahidi tu kuitangaza ndoa. Kama kuoa mke wa zaidi ya mmoja bila ya kumtaarifu mke/wake/watu wengine.
Inajuzu kwa sababu ndoa imekamilika kuwepo mashahidi kumeifanya si siri tena, imeshatangazwa. Ila ni jambo lisilopendeza kisheria (makruuh)
24
KUOA KWA  NIA YA KUACHA
Mume kuoa na katika mkataba wa ndoa akashurutisha kwamba atamuacha mke katika muda fulani au bila ya kushurutisha lakini tayari ameshaweka nia katika nafsi yake ya kuacha.
Kimsingi ndoa yoyote itakayowekewa mkataba/muda maalum kumalizika kwake haikubaliki kisheria ikiwa imeshurutishwa au kuwekwa nia kwani inakuwa ndoa ya muda maalum. Na kuwepo ndani yake hadaa na udanganyifu.
Haijuzu kwa rai ya Jamhuur kwa sababu ya kuwekewa muda wa kumalizika na udanganyifu.

Itaweza kujuzu kwa rai ya Abu Haniyfah ikiwa shurti litabatilishwa na kutenguliwa


Ni muhimu kwa kila Muislamu kuzifahamu vyema aina hizi na kuhakikisha ndoa yake imefungwa katika misingi na taratibu zilizo sahihi. Na kama ni miongoni mwa watakaosimamia au kuwakilisha katika ndoa wazingatie maelezo haya ili waweze kuwa na uelevu katika mwenendo mzima wa ndoa kuepuka matatizo na kuepukana na ndoa zenye utata.

Pia kuwepo tayari kuusimamia ukweli na haki pale ambapo ndoa iliyofungwa ilifungwa katika misingi isiyokuwa sahihi au baadhi ya taratibu zake kukiukwa.

Ikiwa ndoa ni moja katika alama zake Allah Subhaanahu Wata’ala na miujiza yake hatuna budi Waislamu kuhakikisha kuzithibitisha alama hizi kwa kuifunga katika misingi na taratibu sahihi za kisheria. 

Na Allah Ndiye Ajuaye zaidi