31 May 2011

Tuishi Kiislam

Tofauti yetu na wasio kuwa Waislam si chengine kipya ila ni tabia. Uzuri wa mwenendo wa maisha yetu ndio utakaotupatia sifa mbele ya jamii isiyokuwa ya Waislam. Hima yetu ya kutosema uongo na kufuata maadili ya ajabu ndio utakuwa msingi imara wa imani yetu. Haya yote yameelezwa na Habiybul Mustwafaa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa hakuletwa yeye isipokuwa kurekebisha jamii kuwa na tabia njema.

Hakika Uislamu wetu umekamilika kwa kuwa na tabia bora za kuigwa na Waislam wenyewe kwa ushahidi wa Qur-aan na Sunnah.

Kama kweli sisi ni Waislam tunaoipenda diyn yetu ni lazima tuwe tayari kuanza kubadilika kila hatua ya maisha yetu kwa kuishi Kiislam. Zingatio letu litatupeleka hatua baada ya hatua ili kurekebisha nyumba iliyojikita kwenye masuala yasioendana kabisa na mila zetu sisi Waislam.


1. TUZUNGUMZE KIISLAM

Muislam wa kweli ni lazima awe ni mkweli, hatakiwi kuzua uongo, kufitinisha, kusengenya wala kuzungumza kwa sauti ya juu. Haya tunayapata ndani ya Qur-aan:

{{Na uteremshe sauti yako; bila shaka sauti ya punda ni mbaya kuliko sauti zote (kwa makelele yake ya bure).}} [Surat Luqmaan: 19]

Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana kushikamana katika kusema ukweli:

“Shikamaneni na ukweli, kwani ukweli unapeleka katika wema, na wema unapeleka Peponi.” [Muslim]


2. TULE KIISLAM

Muislam anatakiwa ale kilicho mbele yake kwa kutumia mkono wa kulia na asiwe na papara ya kusukuma tonge namna ya kima anavyokula. Aanze kula kwa kusema “BismiLlaah” na amalize kwa kusema “AlhamduliLlaah”. Chakula cha Muislam ni lazima kiwe ni cha halali, hatakiwi kula ovyo ovyo kama wanavyofanya wasiokuwa Waislam. Anapokula aligawe tumbo lake kwenye thuluthi tatu. Thuluthi moja ni ya chakula, nyengine ni ya maji na mwisho ni hewa. Hii ni kwa mujibu wa dalili ya Hadityh:

"Kama ukilazimika kula hakikisha theluthi moja ya tumbo lako unaijaza chakula, theluthi moja maji na acha theluthi moja kwa ajili ya hewa (yaani iache tupu)” (At-Tirmidhiy).


3. TUSIKILIZE KIISLAM

Muziki ni haramu na haifai kwa Muislam kuutengeneza, kutengenezewa, kuimba, kuimbiwa, kuutangaza, kuupeleka muziki, kuuza, kula thamani yake, kununua na kuuza. Muziki umekuwa ni tatizo kubwa kwa Waislam kwani wengine hata usingizi hawapati bila ya kusikiliza muziki. Nyumba za Kiislam sasa zimekuwa sawa na magofu kwa kutopatikana maadili ya Kiislam. Kwani wengi wanaishi tofauti na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni muhimu kwa Waislam wakawa wanasoma Qur-aan kila siku kwa sauti na kwa kusikilizana kwa mtindo wa dawaar (mmoja baada ya mwengine). Tuzibadilishe nyumba zetu kwa kusikiliza idhaa za Kiislam zisizokuwa na mambo ya uchafu na uzushi.

((Na soma Qur-aan kwa utaratibu na utungo))  [Al-Muzammil 73: 4]

Muislam anayesoma Qur-aan atakuwa pamoja na Malaika na Mitume (‘Alayhi swalaatu was-salaam). Hata yule asiyejua kusoma Qur-aan ni vyema akawa na jitihada ya kujifundisha ilhali anakosea au hata kuchekwa. Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Yule ambaye kwamba anasoma Qur-aan naye ni mjuzi (hana shida aina yoyote) atakuwa pamoja na Malaika na Mitume (‘Alayhi swalaatu was-salaam) na watiifu. Na yule ambaye kwamba anarudia pamoja na kuwa na shida katika kusoma basi atakuwa na ujira mara mbili(( [al-Bukhaariy, Muslim, Tirmidhy na Ibn Maajah kutoka kwa ‘Aishah (Radhiya Allaahu 'anha)]


4. TUVAE NA TUTEMBEE KIISLAM

Maringo ya kutembea bila ya shaka yanatokana na mtu kuvaa nguo za kifakhari ambazo hazitakiwi kuvaliwa kwa Muislam. Muislam wa kiume anatakiwa avae nguo zisizoburura. Mwanamke hatakiwi kuonekana zaidi ya viganja vya mikono na kipaji cha sura yake. Mapambo yote ni halali kwa mumewe na walio Maharimu wake. Haitakikani Muislam kutembea kwa kujivuna, kujifakharisha na maringo. Hivi sivyo Uislam unavyotufundisha kuishi. Qur-aan inasema:

{{Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala huwezi kufikia urefu wa milima}} [Surat Israa: 37]

Usiwaangalie watu kwa jeuri au kwa upande mmoja wa uso. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

{{Wala usiwatazame (usiwafanyie watu jeuri), kwa upande mmoja wa uso, wala usende katika ardhi kwa maringo, hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila ajivunaye, ajifaharishaye.}} [Surat Luqmaan:18]
                                      

5. TUJENGE URAFIKI WA KIISLAM

Miongoni mwa matatizo makubwa ya vijana wetu pamoja na Waislam kukosa maadili ya Kiislam ni kuwa na marafiki wasiokuwa na maadili mema. Ni vyema Muislam akawa hana rafiki hata mmoja kuliko kuwa na marafiki kumi wasioishi Kiislam. Kuishi Kiislam yatakikana juhudi na inaanza kwa kuwa na rafiki mwema atakayekukemea unapofanya kosa na kukupa maneno ya subra wakati wa huzuni.

Lazima tuchague marafiki ambao wako radhi na dini yetu na tuepukane na wale ambao hawako radhi na dini yetu. Na tukiona marafiki zetu matendo yao sio mazuri, ni lazima tuepukane nao kwa sababu tunaweza tukaiga tabia zao ambazo zinakwenda kinyume na dini yetu.
Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mtu yamkini kufuata dini ya rafiki yake, kwa hivyo muangalie unayemfanya rafiki.”  (Abuu Daawuud na Tirmidhiy)

6. TULALE KIISLAM

Tumalizie kwa kuona namna anavyotakiwa Muislam kuimaliza siku yake kwa kujipumzisha Kiislam. Muislam anatakiwa atie wudhuu kabla ya kulala, wudhuu unaendana na Sunnah ya kupiga mswaki. Ni vizuri ukaswali rakaa tatu za witri (kwa wasioamka usiku).

Alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akienda kulala usiku anakusanya viganja vyake kisha akivipuliza na akivisomea Suratul-Ikhlaas, na Suratul-Falaq, na Suratu-Nnaas, kisha akipangusa kwa hivyo viganja vyake kiasi anachoweza katika mwili wake, akianza kichwani na usoni na mbele (akifanya hivyo mara tatu).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ukienda kulala soma Ayatul-Kursiy mpaka uimalize kwani Mwenyezi Mungu Ataendelea kukuhifadhi wala hakukaribii shetani mpaka asubuhi”
Unapolala ulaze ubavu kwa upande wa kulia na usome du’aa ifuatayo:

اللّهُـمَّ أَسْـلَمْتُ نَفْـسي إِلَـيْكَ، وَفَوَّضْـتُ أَمْـري إِلَـيْكَ، وَوَجَّـهْتُ وا جْـهي إِلَـيْكَ، وَأَلْـجَـاْتُ ظَهـري إِلَـيْكَ، رَغْبَـةً وَرَهْـبَةً إِلَـيْكَ، لا مَلْجَـأَ وَلا مَنْـجـا مِنْـكَ إِلاّ إِلَـيْكَ، آمَنْـتُ بِكِتـابِكَ الّـذي أَنْزَلْـتَ وَبِنَبِـيِّـكَ الّـذي أَرْسَلْـت
“Ewe Mwenyezi Mungu  nimeisalimisha nafsi yangu kwako, na nimekuachia mambo yangu Wewe na nimeuelekeza uso wangu kwako na nimeutegemeza mgongo wangu kwako, kwa matarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila kwako, nimekiamini kitabu chako ulichokiteremsha na Mtume wako uliyemtuma”.
Bila ya shaka tutakapoishi Kiislam tutakuwa mbali na wasiokuwa Waislam. Hivyo maisha yetu yatakuwa hakika ni ya Kiislam. Kila kitu yatakikana juhudi na inaanza kwa nafsi kujifunga kukubali mafundisho ya Kiislam. Inawezekana kubadilika kwa kuishi Kiislam. Anza sasa, katu usichelewe kuishi Kiislam.

 Nyiradi za kulala
(99)
Alikuwa Mtume صلى الله عليه وسلم akienda kulala usiku anakusanya viganja vyake kisha akivipuliza na akivisomea Suratul-Ikhlaas, na Suratul-Falaq, na Suratu-Nnas, kisha akipangusa kwa hivyo viganja vyake kiasi anachoweza katika mwili wake, akianza kichwani na usoni na mbele .
(akifanya hivyo mara tatu)

(100)
Mtume صلى الله عليه وسلم amesema : “Ukienda kulala soma Ayatul-Kursiy mpaka uimalize kwani  Mwenyezi Mungu  ataendelea kukuhifadhi wala hakukaribii shetani mpaka asubuhi”
)اللّهُ لا إلهَ إلاّ هُـوَ الـحَيُّ القَيّـومُ لا تَأْخُـذُهُ سِنَـةٌ وَلا نَـوْمٌ …..(
(Suratul Baqara -255)

(101)
Amesema Mtume صلى  الله عليه وسلم“Anaesoma aya mbili za mwisho wa Suratul-Baqarah usiku zinamtosheleza"
(آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ كُلٌّ آمَنَ بِاللّهِ وَمَلآئِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لاَ نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ وَقَالُواْ سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ ) ( لاَ يُكَلِّفُ اللّهُ نَفْسًا إِلاَّ وُسْعَهَا لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ رَبَّنَا لاَ تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا رَبَّنَا وَلاَ تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا رَبَّنَا وَلاَ تُحَمِّلْنَا مَا لاَ طَاقَةَ لَنَا بِهِ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَآ أَنتَ مَوْلاَنَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِين)
(Suratul Baqarah 285-286)

(102)
Mtume صلى الله عليه وسلم pia amesema : “Akiamka mmoja wenu kutoka usingizini kisha akarudi basi akikukute kitanda kwa shuka yake mara tatu na amtaje Mwenyezi Mungu  kwani hajui kilicho kuja baada yake.  Na Akilala aseme:
بِاسْمِكَ رَبِّـي وَضَعْـتُ جَنْـبي ، وَبِكَ أَرْفَعُـه، فَإِن أَمْسَـكْتَ نَفْسـي فارْحَـمْها ، وَإِنْ أَرْسَلْتَـها فاحْفَظْـها بِمـا تَحْفَـظُ بِه عِبـادَكَ الصّـالِحـين
“Kwa jina lako Mola wangu, nimeweka ubavu wangu na kwa ajili yako nitaunyanyua, na ukiizuia (ukiichukuwa) roho yangu basi  irehemu na ukiirudisha basi ihifadhi kwa kile unacho wahifadhi nacho waja wako wema”
(103)
اللّهُـمَّ  إِنَّـكَ خَلَـقْتَ نَفْسـي  وَأَنْـتَ تَوَفّـاهـا لَكَ ممَـاتـها وَمَحْـياها ، إِنْ أَحْيَيْـتَها فاحْفَظْـها ، وَإِنْ أَمَتَّـها فَاغْفِـرْ لَـها . اللّهُـمَّ  إِنَّـي أَسْـأَلُـكَ العـافِـيَة
“Ewe Mwenyezi Mungu  hakika Wewe umeiumba nafsi yangu nawe utaiua, ni kwako uhai wa nafsi yangu na ufaji wake, ukiipa uhai basi ihifadhi, na ukiifisha (ukiiua) basi isamehe.  Ewe Mwenyezi Mungu  hakika mimi nakuomba afya njema”

(104)
Alikuwa Mtume صلى الله عليه وسلم akitaka kulala anaweka mkono wake wa kulia chini ya shavu lake  kisha anasema:
اللّهُـمَّ قِنـي عَذابَـكَ يَـوْمَ تَبْـعَثُ عِبـادَك
“Ewe Mwenyezi Mungu  nikinge mimi kwa adhabu yako siku utakayo wafufua waja wako”
(mara tatu)

(105)
بِاسْـمِكَ اللّهُـمَّ أَمـوتُ وَأَحْـيا
“Kwa jina lako Ewe Mwenyezi Mungu  ninakufa na ninakuwa hai”
(106)
Mtume صلى الله عليه وسلم amesema : “Hivi  niwafahamishe juu ya kitu ambacho ni bora zaidi kuliko mtumishi wakati munapolala;  Msabihini Mwenyezi Mungu   mara thelathini na tatu, kisha msifuni Mwenyezi Mungu  mara thelathini na tatu, na kisha mtukuzeni mara thelathini na tatu kwani kufanya hivi ni bora kwenu kuliko mtumishi”
سُبْـحانَ الله
“Ametakasika Mwenyezi Mungu"
(Mara thelathini na tatu )
 أَلْحَمْدُ لِلَّه
“Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu"
(Mara thelathini na tatu )
اللَّه أكْبَرُ
“Mwenyezi Mungu  Mkubwa”
(Mara thelathini na tatu )

(107)
اللّهُـمَّ رَبَّ السّمـواتِ السَّبْـعِ وَرَبَّ العَـرْشِ العَظـيم ، رَبَّنـا وَرَبَّ كُـلِّ شَـيء ، فالِـقَ الحَـبِّ وَالنَّـوى ، وَمُـنَزِّلَ التَّـوْراةِ وَالإنْجـيل ، والفُـرْقان ، أَعـوذُ بِـكَ مِن شَـرِّ كُـلِّ شَـيءٍ أَنْـتَ آخِـذٌ بِنـاصِـيَتِه . اللّهُـمَّ أَنْـتَ الأوَّلُ فَلَـيسَ قَبْـلَكَ شَيء ، وَأَنْـتَ الآخِـرُفَلَـيسَ بَعْـدَكَ شَيء ، وَأَنْـتَ الظّـاهِـرُفَلَـيْسَ فَـوْقَـكَ شَيء ، وَأَنْـتَ الْبـاطِـنُ فَلَـيْسَ دونَـكَ شَيء ، اقـْضِ عَنّـا الـدَّيْـنَ وَأَغْـنِنـا مِنَ الفَـقْر
“Ewe Mwenyezi Mungu  Mola wa mbingu saba na Mola wa arshi tukufu, Mola wetu na Mola wa kila kitu Mwenye kuichanua tembe ya mbegu na kokwa na alieteremsha Taurat na Ijiil na Qur’ani, najikinga kwako kutokana na shari ya kila kitu.   Wewe  ndie mwenye kukamata utosi wake. Ewe Mwenyezi Mungu  Wewe ndie wa Mwanzo hakuna kabla yako kitu, nawe ndie wa Mwisho,hakuna baada yako kitu, nawewe ndie uliewazi, hakuna juu yako kitu chochote na Wewe ndie uliefichika hakuna kilichojificha chini yako. Tulipie madeni yetu na utuepushe na ufakiri”

(108)
الـحَمْدُ للهِ الَّذي أَطْـعَمَنا وَسَقـانا، وَكَفـانا، وَآوانا، فَكَـمْ مِمَّـنْ لا كـافِيَ لَـهُ وَلا مُـؤْوي
“Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu  ambae ametulisha na ametunywesha na akatutosheleza na akatuhifadhi, ni wangapi ambao hawana wa kuwatosheleza wala wa kuwahifadhi”

(109)
اللّهُـمَّ عالِـمَ الغَـيبِ وَالشّـهادةِ فاطِـرَ السّماواتِ وَالأرْضِ رَبَّ كُـلِّ شَـيءٍ وَمَليـكَه، أَشْهـدُ أَنْ لا إِلـهَ إِلاّ أَنْت، أَعـوذُ بِكَ مِن شَـرِّ   نَفْسـي، وَمِن شَـرِّ الشَّيْـطانِ وَشِـرْكِه، وَأَنْ أَقْتَـرِفَ عَلـى  نَفْسـي  سوءاً أَوْ أَجُـرَّهُ إِلـى مُسْـلِم .
“Ewe Mwenyezi Mungu mjuzi wa yaliyojificha na yaliyowazi, Muumba wa mbingu na ardhi, mola wa kila kitu na Mfalme wake, nakiri kwamba hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe, najilinda kwako na shari ya nafsi yangu na shari ya shetani na shirki yake na kujichumia uovu kwa nafsi yangu au kumletea Muislamu.

(110)
Mtume صلى الله عليه وسلم alikuwa halali mpaka asome Suratu-Sajda na Suratul-Mulk .

 Ukitaka kulala tawadha udhu kama wa swala kisha lalia ubavu wako wa kulia kisha sema :
اللّهُـمَّ أَسْـلَمْتُ نَفْـسي إِلَـيْكَ، وَفَوَّضْـتُ أَمْـري إِلَـيْكَ، وَوَجَّـهْتُ وَجْـهي إِلَـيْكَ، وَأَلْـجَـاْتُ ظَهـري إِلَـيْكَ، رَغْبَـةً وَرَهْـبَةً إِلَـيْكَ، لا مَلْجَـأَ وَلا مَنْـجـا مِنْـكَ إِلاّ إِلَـيْكَ، آمَنْـتُ بِكِتـابِكَ الّـذي أَنْزَلْـتَ وَبِنَبِـيِّـكَ الّـذي أَرْسَلْـت
“Ewe Mwenyezi Mungu  nimeisalimisha nafsi yangu kwako, na nimekuachia mambo yangu Wewe na nime uelekeza uso wangu kwako na nimeutegemeza mgongo wangu kwako, kwa matajarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila kwako, nimekiamini kitabu chako ulicho kiteremsha na Mtume wako uliyemtuma”

Ameseme Mtume صلى الله عليه وسلم ‘kwa mwenye kusema haya kisha ukifa utakuwa umekufa katika Uislamu’

No comments:

Post a Comment