Hija ni ibada inayokusanya mambo mengi yanayomkurubisha mja kwa Mola wake Karima. Ni shule ya kutoa malezi na maarifa kwa waja kwa msingi wa tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu.
Safari ya Hija huanza kwa kuwekwa nia safi na ikhlasi na kukamilika kwa ibada na amali makhsusi.
Kwa mara nyingine tena imewadia safari ya uja na mapenzi kuelekea katika ardhi tukufu ya Makka kwa ajili ya kutekeleza ibada tukufu ya Hija. Ni safari fupi lakini iliyojaa nembo na siri kubwa. Ni safari ya siku chache lakini yenye matunda na manufaa makubwa mno. Ni safari ambayo wenye uwezo wa kifedha na kiafya ndio wanaoweza kuitekeleza baada ya kupata tawfiki ya Mwenyezi Mungu. Ni safari ya kuelekea katika kitovu cha Wahyi; ardhi ambazo ni mahala pa maarifa , mlima wa mahaba na mahala pa uja na unyenyekevu.
Mbali na kutekeleza ibada ya kimaanawi na kisiasa ya ibada ya Hija, akiwa Makka hujaji hupata fursa ya kujionea athari muhimu za Uislamu. Katika safari hii ya kimaanawi Hujaji hupata nafasi ya kunufaika kihistoria na kimaanawi na athari za Uislamu katika mji wa Makka na Madina.
Kwa hakika al-Kaaba ni nyumba ya Mwenyezi Mungu iliyobarikiwa na yenye uongofu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 96 ya Surat al-Imran kwamba, “Hakika Nyumba ya kwanza walio wekewa watu kwa ajili ya ibada ni ile iliyoko Makka, iliyobarikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote.”
Wanahistoria wana kauli moja kuhusiana na kujengwa nyumba ya al-Kaaba katika zama za Nabii Adam AS. Imekuja katika kitabu cha Taarikh al-Yaaqubi kwamba, baada ya Nabii Adam kumaliza kujenga al-Kaaba alifanya tawafu. Katika kipindi chote cha historia, Kaaba ikawa ni mahala pa kufanya ibada kwa manabii wengi wa Mwenyezi Mungu.
Nabii Ibrahim aliamrishwa na Mwenyezi Mungu aikarabati al-Kaaba. Mwenyezi Mungu anasema katika aya za 26 na 27 za Surat al-Haj kwamba, “Na pale tulipomweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba tukamwambia: Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kut’ufu, na wanaokaa hapo kwa ibada, na wanao rukuu, na wanaosujudu. Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.”
Nafasi muhimu iliyobainishwa na Qur’ani kuhusiana na al-Kaaba ni ile hidaya na kuongoza kwake watu.
Mwanzoni mwa Uislamu al-Kaaba hakikuwa kibla cha Waislamu. Kwa muda wa miaka kumi na tatu aliyokuwa mjini Makka na muda kidogo mjini Madina, Mtume SAW na wafuasi wake walikuwa wakisali ibada zao wakielekea Baytul Muqaddas.
Hii ni katika halia ambayo, wananchi wa Makka walikuwa wameigeuza Kaaba na kuwa nyumba ya waabudu masanamu.
Nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba ina nafasi muhimu katika ibada za Kiislamu na vile vile uhai wa kijamii wa Waislamu. Waislamu kwa siku huelekea mara tano upande wa al-Kaaba wakati wa kusali. Hii kwamba, kwa siku mamilioni ya watu usiku na mchana na kwa wakati maalumu tena kwa pamoja husali na kuelekea upande wa al-Kaaba, kwa hakika hili ni jambo ambalo huzifanya nyoyo za Waislamu kuwa pamoja na kuzikurubisha zaidi.
Mwenyezi Mungu amewataka Waislamu popote watakapokuwa kuelekea upande wa Makka wakati wa ibada zao, kwa sababu nyumba ya al-Kaaba daima inapaswa kuwa mhimili na kitovu cha kukusanyika wanatawhidi wote.
Fadhila muhimu ya Al-Kaaba ni kuwa, nyumba hii, ni nyumba ya tawhidi na haina msukukumo mwingine usiokuwa wa Kimwenyezi Mungu katika kupatikana kwake na katika kuendelea kwake kuweko.
Mahujaji wakiwa katika nyumba ya Mwenyezi Mungu hufanya tawafu katika mahala ambapo malaika wanatufu na mahala ambapo Mitume wa Mwenyezi Mungu na mawalii wake walikuwa kando ya eneo hilo na kumhimidi Mwenyezi Mungu.
Bwana Mtume SAW anasema: Mwenyezi Mungu anajifakharisha na watu wanaofanya tawafu, na laiti ingelikuwa imeamuliwa kwamba, malaika wapeane mikono na mtu, basi wangepeana mikono na wenye kufanya tawafu katika nyumba ya Mwenyezi Mungu.
Kaaba ni mahala pa amani na usalama kwa wanaadamu wote. Mwenyezi Mungu anasema katika Suratul Baqara aya ya 125 kwamba,
“Na kumbukeni tulipo ifanya ile Nyumba (ya Alkaaba) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani.”
Hivyo basi kila mtu atakayekuwa kando ya Kaaba, anakuwa yuko katika amani kimwili na kiroho na huwa na utulivu.
Usalama na amani ya Nyumba hii ya Mwenyezi Mungu unatokana na dua aliyoiomba Nabii Ibrahimn AS kama inavyosema aya ya 126 ya Suratul Baqarah, “Na alipo sema Ibrahim: Ee Mola wangu Mlezi! Ufanye huu uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda, wale wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.”
Mwenyezi Mungu aliijibu dua ya Ibrahim AS. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kwa karne nyingi, al-Kaaba imesalimika na shari ya waitakiao mabaya. Kisa cha Abraha na jeshi lake la askari waliokuwa wamepanda tembo ni jambo linaloweka wazi uhakika huu.
Abraha Aliyeandaa jeshi kubwa lililokuwa limesheheni tembo wengi ili kwenda kuivunja al-Kaaba na yeye mwenyewe alikuwa amempanda tembo mkubwa sana kuliko wote alikumbwa na hatima mbaya. Waarabu wa Makka waliliogopa sana jeshi lile. Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu alilishushia jeshi la Abraha, jeshi la ndege lililodondosha mawe. Mtu yeyote aliyepatwa na jiwe alisagikasagika yeye na tembo wake na kuwa kama majani yaliyoliwa na kutapikwa kama tunavyosoma katika Qur’ani.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullah WabarakaatuhHivyo basi Kaaba ni nembo ya wanatawhidi na wampwekeshao Mwenyezi Mungu na jambo hilo lilikuwa hivyo katika kipindi chote cha historia.
No comments:
Post a Comment