4 Jul 2011

Hadith ya Mume Muhammad (SAW)

KUJA KWA JIBRIIL عليه السلام KUWAFUNDISHA WAISLAMU MAMBO YA DINI YAO

الحديث الثاني
“مجىء جبريل ليعلم المسلمين أمر دينهم”
عَن عُمَر رضي اللهُ عنه أَيْضاً قال:   بَيْنَما نَحْنُ جُلْوسٌ عِنْدَ رسُولِ الله صلى الله عليه وسلم ذات يَوْم  إذْ طَلَعَ عَلَيْنَا رَجُلٌ شَدِيدُ بَياضِ الثِّيَاِبِ شَديدُ سَوَادِ الشَّعْرِ، لا يُرَى عليه أَثَرُ السَّفَرِ ولا يَعْرِفُهُ مِنَّا أَحَدٌ، حَتى جَلَسَ إلى النَّبِّي صلى الله عليه وسلم، فأسْنَدَ رُكْبَتَيْهِ إلى رُكْبَتَيْهِ ووَضَعَ كَفَّيْهِ على فَخِذَيْهِ، وقال: يا محمَّدُ أَخْبرني عَن الإسلامِ، فقالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم:(( الإسلامُ أَنْ تَشْهَدَ أَنْ لا إلهَ إلا اللهُ وأَنَّ محمِّداً رسولُ الله، وتُقِيمَ الصَّلاةَ، وتُؤتيَ الزَّكاةَ، وتَصُومَ رَمَضان، وتَحُجَّ الْبَيْتَ إن اسْتَطَعتَ إليه سَبيلاً)). قالَ صَدَقْتَ. فَعَجِبْنا لهُ يَسْأَلُهُ ويُصَدِّقُهُ، قال : فَأَخْبرني عن الإِيمان. قال: ((أَن تُؤمِنَ باللهِ، وملائِكَتِهِ وكُتُبِهِ، ورسُلِهِ، واليَوْمِ الآخِرِ، وتُؤمِنَ بالْقَدَرِ خَيْرِهِ وشَرِّهِ)) قال صدقت. قال : فأخْبرني عَنِ الإحْسانِ. قال:(( أنْ تَعْبُدَ الله كَأَنَّكَ تَرَاهُ فإنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فإنَّهُ يَرَاك)). قال: فأَخبرني عَنِ السَّاعةِ، قال: ((ما المَسْؤولُ عنها بأَعْلَمَ مِنَ السَّائِلِ )). قال: فأخبرني عَنْ أَمَارَتِها، قال:(( أن تَلِدَ الأمَةُ رَبَّتَها، وأَنْ تَرَى الحُفاةَ العَُراةَ العالَةَ رِعاءَ الشَّاءِ يَتَطَاوَلُونَ في الْبُنْيانِ )) ثُمَّ انْطَلَقَ، فَلَبِثْتُ مَلِيّاً، ثُمَّ قال : ((يا عُمَرُ، أَتَدْرِي مَنِ السَّائِلُ؟)) قُلْتُ: اللهُ ورسُولُهُ أَعلَمُ . قال:(( فإِنَّهُ جِبْرِيلُ أَتاكُمْ يُعَلِّمُكُمْ دِينَكُمْ))
رَوَاهُ مُسْلِمٌ
KUJA KWA JIBRIIL عليه السلام KUWAFUNDISHA WAISLAMU MAMBO YA DINI YAO

Kutoka kwa ‘Umar رضى الله عنه ambaye amesema: Siku moja tulikuwa tumekaa na Mtume صلى الله عليه وسلم  , hapo alitokea  mtu ambaye  nguo zake zilikuwa nyeupe pepe na nywele zake zilikuwa nyeusi sana; hakuwa na alama  ya machofu ya safari na wala hapakuwa na hata mmoja katika sisi aliyemtambua. Alienda akakaa karibu na Mtumeصلى الله عليه وسلم akaweka magoti yake karibu na magoti yake (Mtume) na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake kisha akasema; Ewe Muhammad! Niambie kuhusu Uislamu.  Mjumbe wa Allaah  صلى الله عليه وسلمalisema:  Uislamu ni kukiri kuwa hakuna mola isipokuwa  Allaah na Muhammad ni Mjumbe wake, kusimamisha Swalah, kutoa Zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji (Makkah) ukiweza.
(Akasema yule mtu yaani Jibriyl) Umesema kweli. Tulipigwa na mshangao kwa kumuuliza kwake Mtume na kumsadikisha.  Na akasema tena: Niambie  kuhusu Iymaan.  Akasema (Mtume صلى الله عليه وسلم) Ni kumwamini Mwenyeezi-Mungu, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na siku ya Qiyaama, na  kuamini ya kuwa kheri na shari zinatoka Kwake (Allaah سبحانه وتعالى  ). (Akasema Jibriyl): Umesema kweli, akasema hebu nielezee kuhusu Ihsaan.  Akasema Mtume صلى الله عليه وسلم   Ni kumuabudu Allaah سبحانه وتعالى   kama vile unamuona na kama humuoni basi Yeye Anakuona.  Akasema (Jibriyl):  Niambie    kuhusu Qiyaama.  Akajibu (Mtume  صلى الله عليه وسلم : Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile Muulizaji. Kisha akamwambia: Nijulishe alama zake: Akajibu (Mtume صلى الله عليه وسلم): Kijakazi atazaa bibi yake, na utaona wachunga wenda miguu chini, wenda uchi (wasio na uwezo wa kumiliki hata mavazi), mafukara (wasiokuwa hata na sehemu ya kuishi kwa umaskini) wakishindana kujenga majumba ya fahari. Kisha akaondoka (Jibriyl) na nilitulia kidogo (nikitafakari). Kisha akasema Mtume صلى الله عليه وسلم : “Ewe ‘Umar! Je, unamjua ni nani yule aliyekuwa akiuliza? Nikasema: Allaah na Mjumbe wake wanajua zaidi.  Akasema Mtume   صلى الله عليه وسلم: Ni Jibriyl, alikuja kuwafundisha dini yenu.
Imesimuliwa na Muslim

Ustaadh Mazinge vs Donald: Nyama ya Nguruwe na Ngamia


Wabillah tawfiq

Nini Quran na ni ya kina nani - Ustadh Shaffy


Allah Akbar

Mungu wenu ni nani? Mazinge ajibu swali


Jee Yesu ni Mungu?

Kisa cha Nabii Ayoub (mwenye imani na ustahamilivu)

Imetafsiriwa na Ukht Haliymah ‘Abdullaah

Historia ya Ayyuub (katika ujira) inawapa faraja wale wote ambao ni wagonjwa au walionyimwa mali au watoto.
Malaika walikuwa wanajadili hali ya binaadamu, utiifu na uasi wao.
Mmoja wao akasema kwamba Ayyuub ndio mbora wa watu ulimwenguni. Alikuwa Muumin mtiifu, daima akiswali kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alimbariki kwa kuwa tajiri miaka themanini. Muda wote huu hakusahau kumuabudu au kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Alishirikiana katika utajiri wake na maskini na kuwavisha walio uchi.
Shaytwaan hakuamini kwamba kuna mtumishi mkweli kama Ayyuub. Shaytwaan alifikiri kwamba utajiri wake ndio sababu ya ukweli wake, kwa hiyo akamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa uwezo Wake amuondoshee Ayyuub utajiri kwa nia mbaya ya kumpotosha. Allaah Akamuondoshea kumpima Nabii Wake.
Akaonyesha kutokana na upotevu huo kwa kusema utajiri ni wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na namshukuru kwa Aliyoniruzuku na namshukuru kwa Aliyochukua. Akashuka chini kwa kusujudu. Hili lilimfanya Shaytwaan akasirike.
Shaytwaan alijaribu mara mbili kumpoteza Ayyuub baada ya kukosa utajiri wake kwa kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa nguvu zake kumuondoshea watoto na afya. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alisema nitakupa uwezo katika mwili wake, lakini nakutahadharisha kuifikia roho yake, ulimi, moyo, kwa sababu ndani yake inasema uongo kuhusu Imaan ya kweli. Ayyuub akaonyesha mwenendo alioufuata wakati alipochukuliwa utajiri wake.
Shaytwaan aligundua kwamba hawezi kumpoteza Ayyuub, hivyo alimwendea mkewe kumpoteza (kumdanganya), kwa kumkumbusha maisha yao ya zamani (ya utajiri). Shaytwaan alifanikiwa katika kumdanganya mkewe. Hilo lilimpelekea kumlalamikia Ayyuub kuhusu hali waliyo nayo sasa. Hili lilimfanya Ayyuub kuapa kwamba atampiga viboko 100 ikiwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala ) Atamrudishia afya yake. 
Shaytwaan hakufanikiwa katika kumpoteza Ayyuub. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akarudishia vyote Alivyopoteza. Ikabakia kwa Ayyuub sasa kutimiza kiapo chake cha kumpiga fimbo mkewe.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akamuagiza kumpiga mkewe kwa mara moja fimbo 100 za mianzi, kwa Kumuonea huruma huyo mama. Kweli Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ni mwingi wa rehema.
Kisa cha Ayyuub kitakuwa daima ni ukumbusho kwetu sote. Inatakiwa tusome kisa hiki mara kwa mara kwa ajili ya kujikumbusha. Wengi wetu tunalalamika kwa kitu kidogo katika maisha. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alimpa mtihani Ayyuub kwa namna ambayo kweli inatakiwa tujihusishe nayo.
Imani yake na uvumilivu ni kitu ambacho kama sisi ni Waumini wa Kiislamu wa kweli tujaribu na kutekeleza katika maisha yetu, wakati Akitupa mtihani katika hali hizi. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika Qur-aan:
“…Bila shaka tulimkuta ni mwenye subira, mja mwema, kwa hakika alikuwa mnyenyekevu sana.” Swaad: 44

Wakati huu ni lazima tumkumbuke Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) zaidi, kufanya ibaada kwa bidii, na kuwa wenye kushukuru sana badala ya kutoridhika na hali zetu. Inabidi Tumtukuze na Tumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kila hali Atakayotupa majaribio. Kama tunavyojua huu ni wakati ambao Shaytwaan anajaribu kuchezea akili zetu, hisia, na udhaifu wetu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Hawezi kusahau kamwe kumlipa mwenye kumtumikia kwa hiyo kazi kubwa.



Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
“Na (Mtaje) Ayyuub alipomwita Mola wake (akasema) Mimi imenipata dhara Nawe Ndiye Unayerehemu kuliko wote wanaorehemu.
“Basi tukamkubalia (wito wake) na tukamuondolea dhara aliyokuwa nayo, na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao. Ni rehma inayotoka Kwetu, na ukumbusho (mzuri) kwa wafanyao ibaada) Al-Anbiyaa: 83-84.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atupe imaan na uvumilivu wakati wa mitihani, Aamiyn.

Fadhila za mwezi wa Sha'abaan na uzushi wa Nisfu

 Muhammad Baawazir

BismiLLaah WalhamduliLLaah Waswalaatu Wassalaamu ‘alaa RasuuliLLaah, wa ba'ad

Mwezi wa Sha’abaan ni mwezi wa nane katika kalenda ya Kiislam. Na ni mwezi ambao upo katikati ya miezi miwili mitukufu; Rajab na Ramadhaan. Mambo ya kuzingatia katika mwezi huu ni kuweza kupambanua yaliyo sahihi na yaliyozushwa, kwani ingawa kuna fadhila zake mwezi huu lakini pia mengi yaliyoenea na yanayofanywa na watu, ni ya Upotofu.
Ni mwezi ambao Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akifunga sana Swawm za Sunnah kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo kutoka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah عنها رضي الله
 " كان رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم  يصوم حتى نقول لا يفطر، ويفطر حتى نقول لا يصوم، وما رأيت رسول الله استكمل صيام شهر إلا رمضان وما رأيته أكثر صياماً منه في شعبان"    رواه البخاري ومسلم
“Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akifunga hadi tukadhani kuwa hatofungua kamwe, na alikuwa akiacha kufunga hadi tukadhani hatofunga tena. Sijamuona Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akifunga mwezi mzima kama alivyokuwa akifunga Ramadhaan, na sijamuona akifunga mara nyingi kama alivyofunga katika Sha’abaan”   [Al-Bukhaariy na Muslim]

Swawm Na Fadhila Za Mwezi Wa Sha'abaan
Juu ya kwamba Mtume الله عليه وآله وسلم صلى alikuwa akifunga  mara nyingi zaidi katika mwezi wa Sha’abaan kuliko miezi mingine ukiondosha Ramadhaan, kama ambao unafungwa wote, hakuwahi hata mara moja kuufunga mwezi mzima wa Sha’abaan. Na ni jambo ambalo lenye kuchukiza kufanya hivyo kama wanavyotueleza wanachuoni kama kina Ibnul Mubaarak na wengi wengine, pia Swahaba mtukufu Ibn ‘Abbaas anasema ni makruhu kufunga mwezi mzima wa Sha’abaan kwani Mtume wa Allah hakufanya hivyo.
Imepokewa kuwa Ibn ‘Abbaas عنهما رضي الله amesema: ‘‘Mtume wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم hakuwahi kufunga mwezi wowote kikamilifu isipokuwa Ramadhaan. [Al-Bukhaariy]
Kukithirisha kwake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ibada katika mwezi huu wa Sha'abaan, ni kutokana na maelezo yake mwenyewe alipoulizwa na Usaamah bin Zayd رضي الله عنه sababu ya kufunga sana katika mwezi huu alijibu:

 ((ذاك شهر تغفل الناس فيه عنه، بين رجب ورمضان، وهو شهر ترفع فيه الأعمال إلى رب العالمين، وأحب أن يرفع عملي وأنا صائم))
“[Sha'abaan] ni mwezi ambao watu hawautilii sana maanani, ulio kati (ya miezi miwili mitakatifu) Rajab na Ramadhaan, na ni mwezi ambao matendo yanapandishwa kwa Mola wa ulimwengu. Nami napenda matendo yangu yapandishwe na hali nikiwa nimefunga” [An Nasaaiy, at-Targhiyb wat-Tarhiyb, uk. 425].
Hadiyth hii na Hadiyth nyengine za Mjumbe wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم zinahimiza kufanya amali njema pale watu wanapoghafilika na kumkumbuka Allaah na ‘Ibaadah, kama kumkumbuka Allaahسبحانه وتعالى katika sehemu za masoko, maduka na biashara zingine, ambapo watu wameshughulishwa na biashara zao na pia katika nyakati za matatizo.  
Mjumbe wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم amesema: “Ibaadah wakati wa matatizo (fitnah) ni kama uhamiaji (hijrah) kwangu” [Muslim] 
Faida na ubora wa kumuabudu Allaah سبحانه وتعالى wakati watu wameghafilika na kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى zimekuja kwa sababu ‘Ibaadah katika nyakati kama hizo ni ngumu zaidi kuliko kumuabudu Allaah سبحانه وتعالى wakati kila mtu amefungamana na ‘Ibaadah.                    
Kufunga katika mwezi wa Sha'abaan ni mazoezi kabla ya Ramadhaan. Hata hivyo, kufunga mwezi mzima wa Sha'abaan ni Makruhu (hakupendezi) na ni kinyume na Sunnah za Mjumbe wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم.  
Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما  amesema:
“Msiutangulie Ramadhaan kwa (kufunga) siku moja au mbili, ila kwa wale tu wenye mazoea ya kufunga kila mara, na kwa hali hiyo hao wanaweza kufunga (siku hizo)” Al-Bukhaariy
Pia imekatazwa kufunga katika mwisho wa Sha'abaan kwa nia ya kutozikosa siku za mwanzo wa Ramadhaan, isipokuwa kwa wale wenye tabia na mpangilio wa kufunga na ikawa siku za mwisho za Sha'abaan zimetokezea sambamba na siku ambazo mtu yule kawaida huwa anafunga, kama vile za Jumatatu na Alkhamiys au imemkuta akiwa anaendelea kulipa Swawm ya deni.
Imeripotiwa katika Swahiyh Al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه   kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: “Kufunga katika mwisho wa Sha'abban kumekatazwa ili kuweka tofauti kati ya Swawm za Sunnah na Swawm za faradhi.”
Vile vile ni kinga ya kuwakinga watu na kuanguka katika mtego wa Shetani, ambaye amewashawishi watu wa Kitabu kuongeza Swawm zaidi ya zile Allaahسبحانه وتعالى  Alizowafaradhishia. Kwa sababu hiyo hiyo, imekatazwa pia kufunga siku ya ‘Yawmu Shakk”. Siku ya shaka ni ile siku ambayo watu hawana uhakika juu ya kuanza kwa Ramadhaan, kwa sababu ya hali ya mawingu kufunga na mwezi kutoonekana au sababu nyinginezo.
Na Imaam Ibn Rajab رحمه الله amesema: ''Funga katika Sha'abaan ni bora kuliko funga katika masiku matakatifu (ambayo ni Dhul Qa'adah, Dhul Hijjah, Muharram na Rajab zilizotajwa katika Suratut Tawbah Aayah ya 36), na Swawm zilizo bora ni zile (zitambulikazo) ambazo ziko karibu na Ramadhaan, kabla au baada. Hadhi na daraja ya Swawm hizi ni kama ya zile za Swalah za Sunnah za Rawaatib, ambazo huswaliwa kabla na baada ya Swalah za fardhi na ambazo huwa ni vijazilio vya upungufu wa zile Swalah za fardhi. Na hali kama hiyo ndiyo ile ile ya Swawm zitambulikazo ambazo huwa kabla na baada ya Ramadhaan, Kama ambavyo Swalah za Sunnah za Rawaatib zilivyo bora kuliko Swalah zingine za kujitolea (za Sunnah), na hivyo ndivyo Swawm zitambulikazo (zilizo katika miezi) ya kabla na baada ya Ramadhaan zilivyo bora kuliko Swawm nyinginezo.'' Taz. Latwaaif al Ma'arif fiyma li Mawaasim al'aam minal Wadhaaif, cha Ibn Rajab al Hanbaliy.

Nisfu Sha'abaan: Kuna Ukweli Wowote? 
Pamoja na ubora huo na daraja hiyo ya mwezi wa Sha'abaan, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakuihusisha siku maalum katika mwezi wa Sha'abaan kufunga. Alikuwa akifunga kwa wingi iwezekanavyo lakini hakutueleza na wala hakuichagua siku ya tarehe 15 ya Sha'abaan kufunga kutokana na sifa zake alizozitaja hapo nyuma, ila tu ametaja Fadhila za usiku huu kutokana na hadiyth hii ambayo hata hivyo haikutaja kuwa kuna ibada maalum inapaswa ifanyike siku hii au usiku wake.
 عن أبي موسى الأشعري رضي الله عنه عن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((إن الله ليطلع في ليلة النصف من شعبان فيغفر لجميع خلقه إلا لمشرك أو مشاحن))   رواه ابن ماجة وحسنه الألباني في السلسلة الصحيحة  
 Imetoka kwa Abu Muusa Al-Ash'ariy رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kasema: “Allaah سبحانه وتعالى Hutokea Katika usiku wa 15 wa Sha'abaan, na Huwasamehe wote isipokuwa Washirikina na wale wenye uadui kwa wengine.” Ibn Maajah na imesemwa kuwa ni Hadiyth Hasan na Shaykh Al-Albaaniy.
Jambo la kushangaza ni kwamba wengi katika Waislam kwa uchache wa elimu na pia kwa kufuata mafundisho yasiyo sahihi ambayo amesingiziwa nayo Mtume صلى الله عليه وآله وسلم, wameitenga siku hiyo ya Nisfu Sha'abaan kufunga na kusimama kisimamo cha usiku na kusoma nyiradi mbalimbali ambazo wamezitunga na pia kusherehekea kwa namna mbalimbali. Sehemu nyingi ulimwenguni hufanya sherehe na Swawm pamoja na kuswali sana usiku kwa kuiadhimisha siku hiyo ambayo huamini ni ya aina yake.
Kuna waliyoipa jina la Shab-E-Baraat au Laylatul Bara-at (usiku wa kuachiwa huru [na moto], au wa kusamehewa) kama huko bara Hindi, Pakistan na Bangladesh. Na kwengine hujulikana zaidi kwa Nisfu Sha'abaan n.k. ambapo katika siku hiyo wanaamini kuwa ni siku ya kusamehewa kwani Allaah Anawaachia huru waja wake walio motoni kutokana na mojawapo ya Hadiyth zisizo sahihi zilizohusishwa na mwezi huu wa Sha'abaan kama hii
“Mwenyeezi Mungu Anawaachia huru waja wake walio motoni kulingana na idadi ya nywele zilizo katika ngozi za mbuzi/kondoo wa Banu Kalb.”
Vilevile kuna imani potofu kabisa katika siku hii, ambapo kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa kushuka kwa Malaika na Ruuh usiku huo kama ilivyo katika Suratul-Qadr Aayah ya 4, wao wameelewa maana yake ni kuwa Ruuh iliyokusudiwa katika sura hiyo ni roho za wale waliokufa! Na kwamba 'roho' hizo zashushwa na kurejea duniani na kukutana na wake wa wenye hizo roho na jamaa zao wengine. Na kwa sababu hiyo, wale wajane hupika vyakula bora vilivyokuwa vikipendwa na hao waume zao waliokufa kisha huviandaa na kusubiri ziara zao kutoka huko walipo. Baadhi ya watu pia huzuru makaburi katika siku hiyo na kuwaombea msamaha wale wote waliokufa mwezi wa Sha'abaan uliopita na huo walio nao.
Katika Surah hiyo ya Al-Qadr ambayo watu hao wameifasiri na kuielewa kinyume, Allaah سبحانه وتعالى Anasema:
}}تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ{{
{{Huteremka (katika usiku huo wa Qadr) Malaika pamoja na Ruuh kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo}} Al-Qadr: 4.
Kwanza, Aayah hii huelezea Usiku wa Qadr (wa Cheo) ambao ni usiku wa mwezi wa Ramadhaan na sio wa siku au tarehe 15 ya Sha'abaan. Pili, maana ya neno Ruuh katika Aayah hiyo ni Malaika Jibriyl, yaani watashuka Malaika pamoja na Jibriyl (pamoja na kwamba naye ni Malaika ila kutajwa kwake pekee bila kuingizwa katika kundi zima la Malaika hao, ni hadhi yake kuu) na sivyo kama wanavyodhani watu kuwa hiyo Ruuh ni roho za waliokufa (Taz. Tafsiri ya Ibn Kathiyr). Vilevile itikadi ya kwamba roho za waliokufa zitarejea tena ulimwenguni si sahihi kutokana na mafundisho sahihi ya Qur-aan na Sunnah.
Pia wengine wameuhusisha huo usiku wa katikati ya mwezi wa Sha'abaan na maneno 'Laylati-m-Mubaarakatin' (Usiku uliobarikiwa) yaliyo katika Aayah ya 3 katika Suratud-Dukhaan isemayo:
}}إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ{{
{{Kwa yakini tumeteremsha (Qur-aan) katika usiku uliobarikiwa, bila shaka sisi ni waonyaji}} Ad-Dukhaan: 4
Wakifasiri huo usiku uliobarikiwa kuwa ni wa 15 Sha'abaan. Lakini hiyo ni tafsiri potofu kabisa kwani inajulikana wazi bila shaka kuwa 'Laylatim Mubaarakatin' iliyokusudiwa hapo kwenye Surah hiyo ni usiku uliopo katika mwezi wa Ramadhaan. Na kama ilivyo wazi ni kwamba Qur-aan imeteremshwa katika mwezi wa Ramadhaan na si katika mwezi wa Sha'abaan na haswa hiyo tarehe 15. Allaah سبحانه وتعالى Anathibitisha hilo katika Suratul Baqarah:
}}شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ{{
{{Ni mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa (ndani ya mwezi huo) Qur-aan ili uwe uongozi kwa kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongozi na upambanuzi (wa baina ya haki na batili)...}} Al Baqarah: 185
Basi hayo wayasemayo baadhi ya watu kuwa usiku huo ni usiku wa kuamkia mwezi 15 Sha'abaan ambao pia wanauita 'Qismatur Rizq' (Mgao wa riziki) si maneno ya kweli, bali ni uzushi na upotofu uliozoeleka na ambao umeenezwa katika Dini hii tukufu na kuichafua na kuivuruga hadi imekuwa sasa ni vigumu sana kupambanua la batili na la haki katika Dini hii iliyokamilika na isiyo na haja ya nyongeza za waongezao.
Pia du’aa zisomwazo ndani ya usiku huo zina kila aina ya uzushi upinganao na Qur-aan, kama walivyobainisha Wanachuoni wa kutegemewa. Na hayo ya kujikusanya usiku huo na kusoma du’aa hizo na nyiradi mbalimbali ni jambo ambalo halimo katika mafunzo ya Kitabu chetu kitukufu na wala katika Sunnah Sahihi.
Wanachuoni mabingwa wa fani ya Hadiyth wamebaini kuwa hakuna hata Hadiyth moja iliyo sahihi katika Hadiyth zilizozagaa ambazo zinazungumzia fadhila na utukufu wa mwezi wa Sha'abaan au haswa tarehe 15 ya Sha'abaan isipokuwa hiyo iliyotajwa juu ya kwamba Allaah سبحانه وتعالى Hutokea usiku huo na kuwasamehe waja wake isipokuwa waliomshirikisha na wenye uadui. Na zaidi ni kuwa zote ima dhaifu au mawdhu'u (za uongo/ kutungwa). Wanachuoni mbali mbali kama Maimaam Ash-Shawkaaniy, Ibnul Jawziy, Ibnu Hibbaan, Al Qurtubiy رحمهم الله حميعا wamelaumu mno na kuzikana Hadiyth au mapokezi hayo yasiyo sahihi kuhusiana na Sha'abaan au siku hiyo ya Nisfu Sha'abaan. (Rejea vitabu vyao kama Al Fawaaidul Majmu'ah, Maudhu'aatul Kubraa na Tafsiyr al Qurtubiy).
Katika baadhi ya Hadiyth za kutungwa ni kama zile zisemazo,
“Katika siku hii (ya 15 Sha'abaan) Mwenyeezi Mungu Huwaachia huru watu kutoka katika Moto wa Jahannam idadi inayolingana na nywele zilizomo katika kondoo wa kabila la Banu Kalb.” Na Hadiyth hii Imaam At-Tirmidhiy anasema ni mbovu na dhaifu.
Na nyingine inasema:
“Yeyote atakayeswali rakaa kumi na nne za Swalah katika usiku wa tarehe 15 ya Sha'abaan atapata ujira ulio sawa na kufunga Swawm na Hija ya miaka ishirini.”
na pia isemayo:
“Kuwa ubora wa siku hii ni kwa sababu jaala ya mwanaadam ndiyo huwa katika siku hii, pia mipango ya mazazi na vifo hupangwa.”

Na riwaya dhaifu nyinginezo ni kama hizi:
  • “Mwenyeezi Mungu tubarikie katika (mwezi wa) Rajab na Sha'abaan na tufikishie Ramadhaan.”

  • “Ubora wa mwezi wa Sha'abaan (kulinganisha na miezi mingine) ni sawa na ubora wangu kuliko Mitume wengine.”

  • “Ukifika (Ukiwa) usiku wa Sha'abaan basi mswali usiku wake na mfunge mchana wake.”

  • “Masiku matano huwa du'aa hazirejeshwi; Usiku wa mwanzo wa Rajab, na Usiku wa Nisfu Sha'abaan, na Usiku wa Ijumaa, na Usiku wa ('Iyd) Al-Fitwr, na Usiku wa ('Iyd) ya Kuchinja.”

  • “Amenijia Jibriyl ('Alayhis Salaam) na akaniambia kuwa huu Usiku wa Nisfu Sha'abaan Mwenyeezi Mungu Huwatoa kwenye Moto watu kwa idadi ya kila unyoya wa mbuzi/kondoo wa Banu Kalb.”

  • “Ee 'Aliy, atakayeswali katika Usiku wa katikati ya Sha'abaan Swalah ya rakaa mia kwa kusoma Qul Huwa Allahu Ahad mara elfu moja, Mwenyeezi Mungu Atamkidhia mahitaji yake yote ya Usiku huo.”

  • “Atakayesoma katika Usiku wa Nisfu Sha'abaan Qul Huwa Allahu Ahad mara elfu moja Mwenyeezi Mungu Atamtumia Malaika elfu moja watakaomjia kumpa bishara njema.”

  • “Atakayeswali katika Usiku wa Nisfu Sha'abaan rakaa mia tatu akasoma katika kila rakaa Qul Huwa Allahu Ahad mara thelathini, basi atakuwa miongoni mwa kundi litakalopewa shafa’ah ikiwa ni katika watu waliostahiki Moto.”

  • “Sha'abaan ni mwezi wangu.”

  • “Atakayehuisha Usiku wa 'Iyd na Usiku wa Nisfu Sha'abaan hautokufa moyo wake siku zitakapokufa nyoyo.”

  • “Atakayehuisha Masiku matano, atapata pepo; Usiku wa Tarwiyah (katika Hajj), na Usiku wa 'Arafah, na Usiku wa siku ya kuchinja, na Usiku wa 'Iyd Al-Fitwr, na Usiku wa Nisfu Sha'abaan.”

Hadiyth zote hizo hapo juu kwa matamshi hayo, hazina uthibitisho wowote wa usahihi wake kisheria. Kwa hiyo hakuna Hadiyth hata moja sahihi yenye kuthibitisha kuitenga au kuihusisha siku ya tarehe 15 ya Sha'abaan kufanya ‘Ibaadah maalum kama kufunga au kuswali Swalah za usiku (Qiyaamul Layl). Na kufanya hivyo ni uzushi na upotofu ambao unapingana na mafundisho ya kipenzi chetu Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم. Ama kwa yule aliyezoea kuswali Swalah za Usiku kila mara basi haikatazwi kwake kuswali vilevile usiku huo, kisichofaa ni mtu ambaye hana ada ya kuswali Swalah za usiku lakini usiku huo akawa haukosi kwa kuamini kuwa una fadhila kubwa.  
Pia tunapata mafundisho kuwa kutenga siku maalum kwa ibada maalum ni jambo linalokwenda kinyume na sheria, isipokuwa lile lililotajwa au kufundishwa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kama kufunga siku ya 'Ashuraa na siku ya ‘Arafah kwa asiye katika Hija ambazo ametubainishia sababu zake. Lau kama hili la kufunga Nisfu Sha'abaan lingekuwa lina umuhimu na faida kwetu basi angetueleza na angelifanya yeye mwenyewe katika uhai wake. Na kama kuna siku bora katika wiki basi ni Ijumaa na ambayo imependekezwa kwetu kufanya matendo mazuri na pamoja na ubora wake huu Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakutuamrisha tufunge siku hiyo wala kuusimamisha usiku wake kwa Swalah. Na kama ingekuwa inaruhusiwa kama wafanyavyo hao wenye kutenga siku maalum kwa ‘Ibaadah na kuacha masiku yote yaliyobaki ya mwaka mzima, basi ingekuwa ni awlaa kwa Mtume wa Mwenyeezi Mungu صلى الله عليه وآله وسلم kutusisitiza tulifanye hilo katika siku ya Ijumaa kutokana na ubora wake. Lakini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakufanya hivyo.
Mwenyewe Mtume صلى الله عليه وآله وسلم anasema: “Msitenge Usiku (wa kuamkia) Ijumaa kuutenga na usiku mwengine (wowote) kwa kuswali, na msitenge siku ya Ijumaa miongoni mwa masiku kwa kufunga, ila yule aliyezoea kufunga na funga yake ikaangukia siku hii [Ijumaa].” Muslim
Na hili latuthibitishia wazi kuwa ‘Ibaadah na matendo yote mazuri hayafanywi katika siku fulani au usiku maalum tu na kuachwa nyingine, maana kufanya hivyo hakutatimiza wajibu wa Mja wa kumuabudu Mola wake. Mja hupaswa kumuabudu Mola wake siku zote za umri wa maisha yake yote hadi atakapoiaga dunia, kwani ‘Ibaadah ni kusudio la msingi la kuumbwa kwake. Anasema Allaah سبحانه وتعالى:
}}وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّى يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ{{
{{Na umuabudu Mola wako hadi ikufikie hiyo yakini (Nayo ni mauti)}} Al-Hijr: 99.
Na ndivyo ilivyokuwa ada ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kumuabudu Mwenyeezi Mungu muda wote wa mwaka mzima, masiku yote, usiku na mchana alitumia katika kumtumikia Allaah  وتعالى سبحانه. 

Ukumbusho Katika Sha'abaan
Iwapo bado unahitajika kulipa Swawm za faradhi za Ramadhaan iliyopita, fanya haraka kulipa kabla ya Ramadhaan nyingine haijafika. Hairuhusiwi kuchelewesha Swawm zilizokosekana mpaka kufikia Ramadhaan inayofuata, isipokuwa katika hali ya ulazima (mfano udhuru unaokubalika ambao umeendelea baina ya Ramadhaan mbili).
Mama wa Waumini 'Aaishah عنها رضي الله amesema,
“Ilikuwa nnazo siku za kulipa za Ramadhaan na sikuweza kuzilipa isipokuwa (katika mwezi wa) Sha'abaan.” Al-Bukhaariy 
Yeyote aliyekuwa na uwezo wa kulipa Swawm zilizompita/ zilizomfutu kabla ya Ramadhaan (ya pili) na asifanye hivyo, basi atalazimika kuzilipa baada ya Ramadhaan (ya pili), na zaidi analazimika kutubia na kumlisha maskini mmoja kwa kila siku iliyompita/ iliyomfutu. [Huu ni msimamo wa Maimam Maalik, Ash-Shafi’iy na Ahmad] na unaoonekana kuwa sahihi zaidi.

Wa Allaahu A’alam

5 Jun 2011

Ibada ya Hijja

Hija ni ibada inayokusanya mambo mengi yanayomkurubisha mja kwa Mola wake Karima. Ni shule ya kutoa malezi na maarifa kwa waja kwa msingi wa tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu.

 Safari ya Hija huanza kwa kuwekwa nia safi na ikhlasi na kukamilika kwa ibada na amali makhsusi.
Kwa mara nyingine tena imewadia safari ya uja na mapenzi kuelekea katika ardhi tukufu ya Makka kwa ajili ya kutekeleza ibada tukufu ya Hija. Ni safari fupi lakini iliyojaa nembo na siri kubwa. Ni safari ya siku chache lakini yenye matunda na manufaa makubwa mno. Ni safari ambayo wenye uwezo wa kifedha na kiafya ndio wanaoweza kuitekeleza baada ya kupata tawfiki ya Mwenyezi Mungu. Ni safari ya kuelekea katika kitovu cha Wahyi; ardhi ambazo ni mahala pa maarifa , mlima wa mahaba na mahala pa uja na unyenyekevu.

Mbali na kutekeleza ibada ya kimaanawi na kisiasa ya ibada ya Hija, akiwa Makka hujaji hupata fursa ya kujionea athari muhimu za Uislamu. Katika safari hii ya kimaanawi Hujaji hupata nafasi ya kunufaika kihistoria na kimaanawi na athari za Uislamu katika mji wa Makka na Madina.
Kwa hakika al-Kaaba ni nyumba ya Mwenyezi Mungu iliyobarikiwa na yenye uongofu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 96 ya Surat al-Imran kwamba, “Hakika Nyumba ya kwanza walio wekewa watu kwa ajili ya ibada ni ile iliyoko Makka, iliyobarikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote.”

Wanahistoria wana kauli moja kuhusiana na kujengwa nyumba ya al-Kaaba katika zama za Nabii Adam AS. Imekuja katika kitabu cha Taarikh al-Yaaqubi kwamba, baada ya Nabii Adam kumaliza kujenga al-Kaaba alifanya tawafu. Katika kipindi chote cha historia, Kaaba ikawa ni mahala pa kufanya ibada kwa manabii wengi wa Mwenyezi Mungu.

 Nabii Ibrahim aliamrishwa na Mwenyezi Mungu aikarabati al-Kaaba. Mwenyezi Mungu anasema katika aya za 26 na 27 za Surat al-Haj kwamba, “Na pale tulipomweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba tukamwambia: Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kut’ufu, na wanaokaa hapo kwa ibada, na wanao rukuu, na wanaosujudu. Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.”


Nafasi muhimu iliyobainishwa na Qur’ani kuhusiana na al-Kaaba ni ile hidaya na kuongoza kwake watu.

Mwanzoni mwa Uislamu al-Kaaba hakikuwa kibla cha Waislamu. Kwa muda wa miaka kumi na tatu aliyokuwa mjini Makka na muda kidogo mjini Madina, Mtume SAW na wafuasi wake walikuwa wakisali ibada zao wakielekea Baytul Muqaddas.

Hii ni katika halia ambayo, wananchi wa Makka walikuwa wameigeuza Kaaba na kuwa nyumba ya waabudu masanamu.

Nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba ina nafasi muhimu katika ibada za Kiislamu na vile vile uhai wa kijamii wa Waislamu. Waislamu kwa siku huelekea mara tano upande wa al-Kaaba wakati wa kusali. Hii kwamba, kwa siku mamilioni ya watu usiku na mchana na kwa wakati maalumu tena kwa pamoja husali na kuelekea upande wa al-Kaaba, kwa hakika hili ni jambo ambalo huzifanya nyoyo za Waislamu kuwa pamoja na kuzikurubisha zaidi.

Mwenyezi Mungu amewataka Waislamu popote watakapokuwa kuelekea upande wa Makka wakati wa ibada zao, kwa sababu nyumba ya al-Kaaba daima inapaswa kuwa mhimili na kitovu cha kukusanyika wanatawhidi wote.

 Fadhila muhimu ya Al-Kaaba ni kuwa, nyumba hii, ni nyumba ya tawhidi na haina msukukumo mwingine usiokuwa wa Kimwenyezi Mungu katika kupatikana kwake na katika kuendelea kwake kuweko.

Mahujaji wakiwa katika nyumba ya Mwenyezi Mungu hufanya tawafu katika mahala ambapo malaika wanatufu na mahala ambapo Mitume wa Mwenyezi Mungu na mawalii wake walikuwa kando ya eneo hilo na kumhimidi Mwenyezi Mungu.

Bwana Mtume SAW anasema: Mwenyezi Mungu anajifakharisha na watu wanaofanya tawafu, na laiti ingelikuwa imeamuliwa kwamba, malaika wapeane mikono na mtu, basi wangepeana mikono na wenye kufanya tawafu katika nyumba ya Mwenyezi Mungu.

 Kaaba ni mahala pa amani na usalama kwa wanaadamu wote. Mwenyezi Mungu anasema katika Suratul Baqara aya ya 125 kwamba,
“Na kumbukeni tulipo ifanya ile Nyumba (ya Alkaaba) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani.”
 Hivyo basi kila mtu atakayekuwa kando ya Kaaba, anakuwa yuko katika amani kimwili na kiroho na huwa na utulivu.

Usalama na amani ya Nyumba hii ya Mwenyezi Mungu unatokana na dua aliyoiomba Nabii Ibrahimn AS kama inavyosema aya ya 126 ya Suratul Baqarah, “Na alipo sema Ibrahim: Ee Mola wangu Mlezi! Ufanye huu uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda, wale wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.”
 Mwenyezi Mungu aliijibu dua ya Ibrahim AS. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kwa karne nyingi, al-Kaaba imesalimika na shari ya waitakiao mabaya. Kisa cha Abraha na jeshi lake la askari waliokuwa wamepanda tembo ni jambo linaloweka wazi uhakika huu.

Abraha Aliyeandaa jeshi kubwa lililokuwa limesheheni tembo wengi ili kwenda kuivunja al-Kaaba na yeye mwenyewe alikuwa amempanda tembo mkubwa sana kuliko wote alikumbwa na hatima mbaya. Waarabu wa Makka waliliogopa sana jeshi lile. Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu alilishushia jeshi la Abraha, jeshi la ndege lililodondosha mawe. Mtu yeyote aliyepatwa na jiwe alisagikasagika yeye na tembo wake na kuwa kama majani yaliyoliwa na kutapikwa kama tunavyosoma katika Qur’ani.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh
Hivyo basi Kaaba ni nembo ya wanatawhidi na wampwekeshao Mwenyezi Mungu na jambo hilo lilikuwa hivyo katika kipindi chote cha historia.

4 Jun 2011

Hadith ya Nabii Muhammad (SAW)




” إنما الأعمال بالنيات “

عن أَمِيرِ المُؤمِنِينَ أَبي حَفْصٍ عُمَرَ بنِ الخطَّابِ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ : سَمِعْتُ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ:   ((إِنَّما الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ وإنَّما لكُلِّ امْرِىءٍ ما نَوَى، فَمَنْ كانَتْ هِجْرَتُهُ إلى اللهِ ورَسُولِهِ فَهِجْرَتُهُ إلى اللهِ ورَسُولِهِ، ومَنْ كانَتْ هِجْرَتُهُ لِدُنْيا يُصِيبُها أو امْرأةٍ يَنْكِحُها فَهِجْرَتُهُ إلى ما هَاجَرَ إليه)).

رَوَاهُ إِمَامَا الْمُحَدِّثِينَ أَبُو عَبْدِ اللهِ مُحَمَّدُ بنُ إِسْمَاعِيل بن إِبْرَاهِيم بن الْمُغِيرَة بن بَرْدِزبَه الْبُخَارِيُّ     وَأَبُو الْحُسَيْنِ مُسْلِمٌ بنُ الْحَجَّاج بن مُسْلِم الْقُشَيْرِيُّ النَّيْسَابُورِيُّ   رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا فِي “صَحِيحَيْهِمَا” اللذينِ هُمَا أَصَحُّ الْكُتُبِ الْمُصَنَّفَةِ.


Kutoka kwa Amiri wa Waumuni, Abu Hafs ‘Umar Ibn Al Khattaab رضى الله عنه ambaye alisema : Nilimsikia Mjumbe wa Mwenyeezi  Mungu صلى الله
عليه وسلم akisema:
Vitendo vinategemea (vinalipwa kwa) nia na kila mtu atapata kwa mujibu wa kile alichokusudia.  Kwa hivyo yule aliyehama  kwa ajili ya Allaah na Mtume wake, uhamaji wake ni kwa ajili ya Allaah na Mtume wake, na  yule ambae uhamaji wake ulikuwa ni kwa ajili ya manufaa ya kidunia au kwa ajili ya kumuoa mwanamke (Fulani)  uhamaji wake ulikuwa kwa kile kilichomuhamisha.

Imesimuliwa na Maimam wawili mabingwa wa hadithi Abu Abdalla Muhammad  Ibn Ismail Ibn Ibrahim Ibn Mughiyra Ibn Bardizbah Al Bukhari na Abu Al Husayn Muslim Ibn Al-Hajjaj Ibn Muslim Al Qushayri An-Naysaburi, katika sahihi zao mbili ambavyo ni vitabu vya kutegemewa.

President Obama admited that he is a Muslim




Mkataa pema pabaya panamwita - Ustadh Rashid Al Shukery


Yarabi tuepushe na majaribu ya Sheitani