5 Aug 2011

Mambo ya kuzingatia katika mwezi mtukufu wa Ramadhan

YANAYOBATILISHA (YANAYOHARIBU) SWAWM
  1. Kula na kunywa kwa makusudi. Na sio kwa kusahau wala kwa bahati mbaya au kwa kulazimishwa, katika mchana wa Swawm.
  2. Kujitapisha kwa makusudi. Kuwe kujitapisha huko kwa kutia kidole mdomoni au kunusa kitu kitachopelekea kutapika.
  3. Mume kumuingilia Mke wake. Na pia kumkumbatia au kumchezea hadi yakamtoka manii.
  4. Kujichua (kuyatoa manii) kwa makusudi ima kwa mkono au kwa kuchezewa na Mkeo au kwa njia yoyote ile. Ama manii hayo yakitoka kwa kuota (ndoto) au kutazama (bila kukusudia) basi haiharibu Swawm.
  5. Kupatwa na Hedhi au Nifasi kwa Mwanamke. Hata kukiwa kutokea huko kuwa ni wakati wa kukaribia kufuturu/kufutari.
  6. Mwenye kutia Nia ya kula wakati amefunga, kwa sharti kuwa kaazimia tendo hilo hata kama hakulitekeleza.
  7. Kudhania kuwa jua lishazama magharibi au bado hakujapambazuka (yaani haujaanza wakati wa kufunga), kisha akala, akanywa au akamuingilia mke wake.

YASIYOBATILISHA (YASIYOHARIBU) SWAWM
  1. Kula au kunywa kwa kusahau, kimakosa au kulazimishwa.
  2. Kuingia maji ndani ya matundu ya mwili bila kukusudia, kwa mfano wakati wa kuoga.
  3. Kudungwa sindano mwilini wakati wa maradhi.
  4. Dawa ya maji idondoshewayo machoni.
  5. Kujipulizia dawa ya asthma mdomoni (puffer au inhaler).
  6. Kuoga na kujimwagia maji mwilini wakati wa joto kali.
  7. Kuonja chakula kwa mpishi kwa sharti asimeze kile akionjacho.
  8. Kumbusu au kumkumbatia mkeo, kwa sharti awe mtu ana uwezo wa kujizuia na kudhibiti matamanio yake.
  9. Kupiga chuku (cupping), ikiwa kupiga chuku huko hakutomfanya huyo mtu adhoofike. Ingawa kuna baadhi ya Maulamaa wanaona kuwa haifai.
  10. Haitobatilika Swawm ya mtu atakayeamka na janaba au atakayeota mchana wa Swawm akatokwa na manii.
  11. Kuingia harufu ya manukato au udi puani mwake. Ingawa baadhi ya Maulamaa wanasema ni vizuri kujiepusha moshi usiingie hadi kufika tumboni.
  12. Kupiga mswaki, kusukutua au kusafisha pua kwa kutia maji puani bila kuzidisha.
DUA YA KUFUTURU/KUFUTARI
عن عبد الله بن عمر رضي الله عنه أن النبي صلى الله عليه وسلم كان إذا أفطر قال: () ذهب الظمأ وابتلت العروق، وثبت الأجر إن شاء الله )) رواه أبو داود والنسائي بإسناد حسن .
Kutoka kwa Abdullaah bin ‘Umar رضي الله عنه ambaye amesema, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipokuwa akifungua, anasema: ((Kiu kimeondoka, na mishipa imelainika, na yamethibiti malipo Mwenyeezi Mungu Akipenda)). Imesimuliwa na ma-Imaam Abu Daawuud na An-Nasaaiy.
KUFUNGUA KWA TENDE AU MAJI
قال رسول الله صلى الله عليه وسلم ((من وجد التمر فليفطر عليه ، ومن لم يجد التمر فليفطر على الماء ، فإن الماء طهور)) رواه أحمد وأبو داود والترمذي
Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Atakayepata tende afuturu kwayo, na asiyepata basi afungue kwa maji, kwani maji ni twahara)) Imesimuliwa na ma-Imaam Ahmad, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy
WATU WALIORUHUSIWA KUTOFUNGA
Kufunga Ramadhaan ni Fardh kwa kila Muislam aliye baaligh, mwenye akili timamu isipokuwa kwa wale kufunga ni shida na itawaletea madhara nao ni wenye udhuru kama huu ufuatao:
  1. Walio katika safari na wagonjwa ambao kufunga kwao kutawafanya wawe wagonjwa zaidi, haipendezwi kwa watu hao kufunga, lakini wakifunga Swawm yao itakubaliwa. Wakichagua au kupenda kuwa wasifunge basi ni lazima walipe siku hizo wasizofunga baada ya Ramadhaan.
  2. Wanawake walio katika hedhi na waliotoka kuzaa ambao wako katika damu ya Nifaas hawaruhusiwi kufunga, na wakifunga katika hali hii, basi Swawm yao haitokubaliwa. Nao pia ni lazima walipe kila siku walizoacha baada ya Ramadhaan.
  3. Wanawake wajawazito na wanaonyonyesha ikiwa watakhofu kuwa Swawm itawadhuru watoto wao au wenyewe, hao sio lazima kufunga. Lakini ikiwa hawatafunga Ramadhaan basi ni lazima wafunge baada ya Ramadhaan kulipa siku zao. Na ikiwa waliacha kufunga kwa sababu tu ya kukhofia afya ya watoto wao, basi wanapaswa kulipa na kumlisha maskini mmoja kwa kila siku moja iliyowapita katika Ramadhaan.
  4. Watu wasioweza kufunga kutokana na umri mkubwa na maradhi yasiyopona hawatakiwi kufunga. Inawatosheleza kulisha maskini mmoja kwa kila siku moja wanayoshindwa kufunga. Na kila wakiweza kulisha maskini zaidi ni bora.
Tunawaombea kila la kheri katika Mwezi Mtukufu Wa Ramadhaan . Allaah Aujaalie uwe wa kheri na mavuno.
Source: Alhidaaya

No comments:

Post a Comment